Mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino
cha Tanzania, SAUT ni mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maboresho
ya sekta ya elimu.
Lengo ni kuwajengea
wahitimu fursa za kuweza kupata ajira sanjari na kupambana na changamoto zinazojitokeza
katika maisha. SAUT inapania kuwaandaa waatalam wenye maadili, utu wema, ari na moyo
wa kujituma ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Jiji la Mungu.
Ni changamoto
iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Evaristi Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, Tanzania,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha SAUT, Tawi la Mbeya wakati wa Ibada
ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa Mwaka wa Masomo 2013-2014. Zaidi
ya wanafunzi 350 wamejiunga na SAUT, Tawi la Mbeya kwa kozi mbali mbali zinazotolewa
Chuoni hapo.
Askofu Chengula imeitaka Jamii kuendeleza maadili na utu wema
kwa kuwaonesha wanafunzi hao ukarimu pamoja na kuwajengea mazingira mazuri yatakayowasaidia
kujikita zaidi katika masomo, daima wakijiandaa kwa maisha bora kwa siku za usoni.
Amewataka wanafunzi kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni
wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba, hali inayowatendea sana kwa kuwaacha katika
utupu na majonzi na madonda ya muda mrefu.
Wakati huo huo, Professa Romwald
Haule amewataka wanafunzi kujifunza kwa bidii, juhudi na maarifa, huku wakionesha
moyo wa unyenyekevu, kwani elimu wanayoipata wakati wakiwa chuoni ni tone tu la maarifa
yanayoweza kupatikana duniani.