Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2013 kutoka kwa Patriak Fouad Twal wa Yerusalemu
Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013, Kanisa linapenda kuonesha
mshikamano wa dhati na wananchi wa Syria wanaoendelea kuteseka kutokana na vita na
kwamba, kuna maelfu ya watu yamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana kuhofia kuhusu
usalama wa mali na maisha yao! Hili ni kundi ambalo linalazimika kuishi kama wakimbizi
katika nchi jirani ziliko kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati.
Kanisa kwa upande
wake, litaendelea kuombea amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu sanjari
na kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa vita na kinzani za kijamii, kisiasa
na kidini huko Masharki ya Kati.
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni,
Kanisa limeendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, jambo ambalo linaendelea
kuzaa matunda ya ushirikiano yanayoonekana kati ya waamini wa dini na madhehebu mbali
mbali ya Kikristo.
Waamini wanaoishi huko Mashariki ya Kati, wana matumaini
makubwa ya kukutana na kuonana na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya
kichungaji katika Nchi Takatifu. Hii itakuwa ni fursa nyingine ya kuweza kuwaimarisha
ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini, licha ya magumu wanayokabiliana nayo
katika hija ya maisha na utume wao kama Wakristo huko Nchi Takatifu. Wapalestina na
Waisraeli wana haki ya kuishi katika Nchi Takatifu.
Huu ni ujumbe wa Patriaki
Fouad Twal wa Yerusalemu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013. Ni
ujumbe unaotoa kwa muhtasari matukio makubwa yaliyojiri katika Kipindi cha Mwaka 2013
unaoyoyoma kwa kasi! Maadhimisho na kufunga Mwaka wa Imani; mateso na mahangaiko ya
wananchi wa Syria, Iraq, Libya na Misri bila kusahau mgogoro wa siku nyingi kati ya
Israeli na Palestina na umuhimu wa kutafuta amani ya kudumu huko Mashariki ya Kati
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake.
Patriaki Fouad Twal anawaalika
wanasiasa kuonesha utashi wa kisiasa, ili kuweza kutafuta suluhu ya kudumu kwa kusitisha
vita ambayo imeendelea kusababisha madhara makubwa kwa maisha na mali ya watu; kwa
kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, kinyume kabisa na mwelekeo
wa sasa unaokumbatia utamaduni wa kifo na madhulumu!
Patriaki Twal anasema,
kwa mara ya kwanza Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox waliweza kuadhimisha Pasaka
siku moja, hapo tarehe 5 Mei 2013, hii ni hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano
ya kiekumene miongoni mwa Makanisa katika masuala ya imani, ili hatimaye, kufikia
umoja kamili kadiri ya mapenzi ya Kristo kwa Kanisa lake.
Patriaki Twal analaani
vitendo vyote vinavyosababishwa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini inayoendelea
kuongezeka siku hadi siku kutokana na chuki za kidini, jambo ambalo halipendezi kwani
linatishia uhuru wa kuabudu ambao ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kanisa katika
Nchi Takatifu, litaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuboresha makazi ya Familia
za Kikristo.