2013-12-21 15:30:00

Tekelezeni dhamana na utumishi wenu kwa kuzingatia: weledi, huduma na utakatifu wa maisha!


Majilio ni kipindi ambacho kina utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na viashiria vya kiliturujia vinavyowaandaa waamini kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, kielelezo makini cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa ajili ya huduma kwa Kanisa; huduma ambayo inafanywa kwa majitoleo makubwa; kwa kuzingatia kipaji cha ugunduzi; kwa kusikiliza na kusikilizana; kwa kujadili na kuheshimiana.

Hizi ni salam na matashi mema ya Noeli kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na wasaidizi wake wa karibu, siku ya Jumamosi, tarehe 21 Desemba 2013. Anawaalika kuendelea kusali na kumwombea Askofu mkuu Pietro Parolin aliyeanza kutekeleza utume wake hivi karibuni kama Katibu mkuu wa Vatican. Anawatakia kheri na baraka wale wote wanaohitimisha huduma na utume wao mjini Vatican tayari kuanza maisha ya pensheni ya uzee, ili kupata muda zaidi wa kusali na kuwahudumia waamini watakaokutana nao!

Baba Mtakatifu anawapongeza viongozi vijana wanaoendelea kutekeleza dhamana na utume wao kwa Kanisa la kiulimwengu kwa kufuata mifano bora ya "Wazee wa Kanisa". Hawa ni vijana wanaofanya kazi kwa ari na moyo mkuu; kwa weledi na umakini wa ajabu, daima wakijitahidi kutekeleza wajibu wao wa kila siku. Baba Mtakatifu anasema, angependa kuwataja kwa majina, lakini anaogopa kwamba, anaweza kusahau wengine na hivyo kushindwa kuwatendea haki na mapendo. Viongozi hawa ni mashahidi muhimu sana katika hija inayotekelezwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anakazia umuhimu wa kutekeleza wajibu si kwa sababu ya ukuu wa kitengo alichokabidhiwa mtu, bali huduma inayozingatia weledi kwa kujikita katika utekelezaji makini wa majukumu, kusoma na kujiendeleza zaidi na zaidi kwani elimu haina mwisho. Hii ni sifa muhimu sana kwa wafanyakazi wa Vatican, jambo linalohitaji msingi thabiti.

Baba Mtakatifu anasema, sifa kuu nyingine ni huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu, Kanisa la kiulimwengu na kwa ajili ya Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia. Kwa wale wanaofanya kazi mjini Vatican wanapaswa kuhisi hali hii badala ya kufanya kazi kwa mazoea, bila kuweka chachu ya maisha yenye mwono na mwelekeo mpana zaidi. Bila kuwa na sifa hizi, wafanyakazi wa Vatican wanakuwa ni mzigo mkubwa wa urasimu usioweza kubebeka; wanageuka na kuwa ni wapelelezi na wachunguzi; watu wasiotoa nafasi kwa Roho Mtakatifu wala ukuaji wa Watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, sifa nyingine kwa wafanyakazi wa Vatican inajikita katika utakatifu wa maisha, moja ya tunu msingi katika maisha ya Kikristo; ubora na huduma. Utakatifu unaonesha ile hali ya mtu kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu; akiwa na moyo wazi kwa ajili ya Mungu; ni hali inayomwezesha mtu kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala; unyenyekevu wa ndani, daima akijitahidi kuwa karibu zaidi na Watu wa Mungu. Hii ni sifa muhimu sana kwa kila Padre.

Baba Mtakatifu anasema, utakatifu wa maisha unaongozwa na dhamiri nyofu ili kufuata ukweli badala ya kukumbatia "maneno ya mitaani au uzushi". Dhamiri nyofu inapaswa kufanyiwa kazi katika uhalisia wa maisha na wala isibaki kuwa ni nadharia tu! Baba Mtakatifu anasema, uzushi unaharibu ubora na sifa ya mtu; unaharibu kazi na mazingira.

Baba Mtakatifu anawaalika wasaidizi wake wa karibu katika hotuba ya matashi mema kwa Siku kuu ya Noeli kumtafakari Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki; mkimya na muhimu sana, aliyekuwa bega kwa bega na Bikira Maria katika hija ya maisha yake hapa duniani; akasimama kidete kutoa ulinzi na tunza kwa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu ni mfano wa huduma kwa Kanisa. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kazi, lakini zaidi kwa sala wanazoendelea kutolea kwa ajili ya maisha na utume wake; hata Yeye anawakumbuka katika sala zake.







All the contents on this site are copyrighted ©.