2013-12-21 16:12:25

Pendekezeni majina ya watu watakaoshiriki katika Bunge maalum la Katiba


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameyaalika na kuyakaribisha makundi mbali mbali katika jamii kupendekeza majina ya watu ambao Rais atayafikiria katika uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Rais Kikwete ametoa mwaliko huo kulingana na mamlaka anayopewa katika Kifungu cha 22(1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83) na aliutangaza rasmi mwaliko huo katika Gazeti la Serikali Na. 443 la Ijumaa iliyopita, Desemba 13, 2013.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam Ijumaa, Desemba 20, 2013 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, mwaliko huo ambao pia utatangazwa katika magazeti ya kawaida, makundi yaliyokaribishwa kutoa mapendekezo yametakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa kila kundi.

Makundi hayo ambayo yametajwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni Taasisi zisizokuwa za Kiserikali, Taasisi za kidini, Vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Taasisi za elimu ya juu, Makundi ya watu wenye ulemavu, Vyama vya wafanyakazi, Vyama vinavyowakilisha wafugaji, Vyama vinavyowakilisha wavuvi, Vyama vya wakulima na Makundi mengine yenye malengo yanayofanana.

Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa katika kuwasilisha mapendekezo ya majina yao, makundi yaliyoalikwa yanalazimika kuonyesha umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya mtu anayependekezwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia. Katika mwaliko wake, Rais Kikwete ameelekeza kuwa orodha ya majina ya wanaopendekezwa, iwasilishwe kwa maandishi ama kwa kupelekwa na mtu kwa mkono ama kwa kutumia huduma ya Posta.








All the contents on this site are copyrighted ©.