Bunge la Tanzania lahitimisha kikao cha 14 kwa "majanga"
Hotuba ya Mheshimiwa Mizengo P. Pinda (MB), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wakati wa kuhitimisha shughuli za mkutano wa 14 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Tarehe 21 desemba, 2013
I: UTANGULIZI Masuala
ya Jumla
Mheshimiwa Spika, Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa Dodoma
kwa takriban siku 15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi za Mkutano
wa 14 wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa hivi leo.
Mheshimiwa
Spika, Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa
Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge
lako Tukufu. Wengi wetu tunafahamu uwezo mkubwa wa Dkt. Asha Rose Migiro na bila
shaka ndiyo sababu Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi wa kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia
sifa nzuri alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje
ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, Tangu Mkutano
wa 13 wa Bunge baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki.
Napenda kutumia fursa hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu
kuungana na Nchi ya Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga ubaguzi
wa rangi, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba Mandela kilichotokea
tarehe 5 Desemba 2013. Wote tunakubaliana kwamba huu ni msiba Mkubwa kwa Dunia nzima
na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na historia yake.
Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuwakilisha vyema Watanzania wote katika
msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima. Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati
wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela tarehe 15 Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa
kuitangaza Tanzania Dunia nzima katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani
Afrika katika Karne ya 20. Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika vizazi
vingi vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na kufuata nyayo zake.
Maswali
Mheshimiwa Spika, Katika Mkutano
huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170 na ya nyongeza 458
ambayo yote yalijibiwa na Serikali. Aidha, maswali 17 ya msingi na 15 ya nyongeza
yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Niwapongeze
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa Mawaziri kutoa
majibu ya maswali hayo kwa umahiri mkubwa.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa
zifuatazo:
Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa Sheria
ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];
Pili: Kujadili
Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge za Sekta Mtambuka.
Tatu: Kujadili
Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma; na
Nne: Kujadili
Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za Kisekta.
Aidha, Bunge
lako Tukufu lilijadili kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada wa Sheria ya Marekebisho
ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The Excise (Management and Tariff) (Amendment)
Bill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 ulisomwa
kwa mara ya kwanza.
Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kujadili Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi mkubwa
na kwa kina. Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa
na Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.
II: KILIMO Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika, Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13, hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini
kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno mazuri
ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya
chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2013 katika maeneo yenye matatizo
ya usalama wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla ya Watu 828,063 wanakabiliwa na
upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi
Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula (NFRA) ulitenga jumla ya Tani 16,119 za chakula cha mgao kwa Halmashauri
zenye mahitaji ya chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya
Tani 13,716 zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika. Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa
na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na Manyoni.
Ninawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula
hicho kufanya hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014. Ambao hawatatekeleza maagizo
haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Wananchi kuwa
Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa chakula katika Halmashauri zenye hali
tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula.
Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na miezi hii kuwa katika kipindi cha mwisho wa msimu wa
ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia sokoni kimeanza kupungua. Hali hii imesababisha
bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika soko hapa Nchini kuanza kupanda
ingawaje si kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi
536.86 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba,
2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 1,188.60
kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa kilo mwezi Novemba, 2013.
Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi
ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile
za kipindi kama hiki mwaka jana. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri
kuendelea kuwahamasisha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya
zao na kuuza ziada katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu.
Halmashauri zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani
na majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa
Spika, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ilipanga
kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea na kazi hiyo na hadi kufikia tarehe
11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499 za nafaka sawa
na Asilimia 87.4 ya kiasi kilichopangwa kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16
Desemba, 2013, Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba
ya jumla ya Tani 233,808 za nafaka. Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani
493 ni za Mtama.
Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yake yaliyoko
katika Mikoa iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye Mikoa yenye
upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha msaada kitakachohitajika
kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9 Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129
za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua
chakula katika Mikoa yenye ziada ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu
wa chakula.
Hali Halisi ya Usambazaji wa Pembejeo
Mheshimiwa
Spika, Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali
ilichapisha jumla ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya pembejeo za Kilimo kwa msimu wa
Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12 Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na Asilimia
96 za mbolea ya kupandia na Tani 42,295 sawa na Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia zilikuwa
zimekwishafikishwa katika Mikoa husika kulingana na aina ya mazao yanayohitaji
mbolea hizo. Aidha, Maghala ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya
kutosha ya mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa
vocha zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya pembejeo inayomlenga
Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.
Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali ilitenga jumla ya Shilingi
Bilioni 109.6 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kununua
Tani 250,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 19 Desemba, 2013 NFRA ilikuwa imenunua
jumla ya Tani 218,499 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 109.25 na kwa ajili hiyo.
Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri ya wastani wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi,
zoezi hilo lilikuwa na matokeo mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita
na liliwavuta Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi
sasa Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya zoezi hilo na imehakikisha
kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa NFRA wamelipwa fedha zao. Aidha, natambua
kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala kukusanya nafaka hiyo kutoka kwa Wakulima na kama
nilivyosema katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali inatambua kuwa Wakala hao kutoka
Mikoa ya Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali
jumla ya Shilingi Bilioni 8.65 Niwaombe Wakala wote wanaoidai Serikali kuendelea kuwa
na subira wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi
cha deni lao lipo ndani ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka
wa fedha wa 2013/2014.
III: MPANGO WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA
Mheshimiwa Spika, Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua
Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial Inclusion
Framework). Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa Uholanzi Mheshimiwa Máxima
Zorreguieta Cerruti ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
katika Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa
Spika,
Lengo la Mpango huo ni kusimamia ukuzaji wa huduma za
kifedha kwa jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya
Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza huduma karibu kwa jamii pana zaidi ya Watanzania
kwa kutumia mifumo ya Teknolojia mbalimbali katika kufikisha huduma za kifedha
kwa Wananchi na hasa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao
wako nje ya mfumo rasmi wa kifedha. Teknolojia hizo ni pamoja na:
Huduma za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent Banking); Huduma
za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL MONEY na
Easy PESA. Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS).
Aidha, Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora kwa kutumia
Sayansi na Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha Sekta ya Fedha
katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa ujumla. Mpango huu pia utawezesha kuongeza
kasi ya upatikanaji wa Chakula, masuala ya Lishe na Maendeleo Vijijini kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika, Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika Nchi mbalimbali
Barani Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo rasmi wa Taasisi za Kifedha
ni Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi waliopo kwenye Mfumo rasmi wa
Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo
(SACCOs) ni Asilimia 22. Asilimia 78 ya Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na
wengi wao ni kutoka Vijijini hasa Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za
Kifedha unalenga kufikia Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha
ifikapo mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, Kiwango hiki
kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa huduma za kifedha unatokana na changamoto
zifuatazo:
Moja: Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha Vijijini ni
hafifu hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za kiusalama; Mbili: Wananchi
wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua umuhimu na faida ya huduma za kifedha.
Aidha, utamaduni wa kujiwekea akiba na kukopa ni mdogo; na. Tatu: Taasisi nyingi
za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini ambao ni Wakulima hawana fedha
za kutosha kuweza kuweka akiba katika Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni
mdogo, hivyo wakipeleka huduma zao huko hawatapata faida. Mheshimiwa Spika, Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi wengi
wa Vijijini hasa Wakulima. Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
Moja: Kuwezesha
Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata mikopo ya kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo
na shughuli nyingine za kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;
Mbili: Huduma
za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi wengi hasa Wakulima kupata mikopo ya pembejeo
na mikopo ya ununuzi wa mazao;
Tatu: Huduma za Kifedha Vijijini ni Mkombozi
wa Makundi maalum kama vile Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia
Wananchi kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo na kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki; na
Nne: Kuwepo
kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza Usalama wa Chakula, kulinda mazingira na
kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri ya kuishi.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imeonesha juhudi kubwa katika kuanzisha Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini kwa mfano
tumeweza kuanzisha Benki nyingi Nchini. Tayari tunazo Benki takriban 52 zenye matawi
zaidi ya 609 kote Nchini. Lakini pia tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi
zaidi ya 27 na Mawakala wa Bima takriban 600. Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma
5, Masoko ya Mitaji na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban 5,600.
Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa kutumia Huduma
za Kifedha kupitia mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala
(POINTS OF SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo zaidi ya 55,000 ambapo
Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment) wanakadiriwa kufika takriban 100,000.
Mheshimiwa
Spika, Maisha bora kwa kila Mtanzania ni pamoja na kutumia Teknolojia
na kurahisisha maisha. Kwa mfano, huduma za M-PESA peke yake zinawezesha malipo kwenye
biashara mbalimbali zaidi ya aina 300 ikiwemo manunuzi kwenye Supermarket na maduka
ya kawaida. Huduma hizo ambazo zinatolewa pia kwa njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY,
EASY PESA zinaweza kulipia Luku, Ada za shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha
huduma zao na Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered,
Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za jumuishi za
kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki kwenda M- PESA, TIGO
PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala. Kwa sasa Watumishi walio Vijijini hawana
tena sababu ya kufunga Ofisi kufuata mishahara Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha
na wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa Watumishi
unaongezaka.
Mheshimiwa Spika, Ni kweli kwamba tunayo
kazi kubwa ya kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini. Lakini ni ukweli
kuwa Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una manufaa makubwa
na mengi ikiwemo kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa kupeleka
maendeleo Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo ya Milenia.
Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha kusonga mbele kwa kasi
kubwa zaidi. Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha na Vituo vya Kifedha kupitia
mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa kutumia Wakala kuongeza jitihada katika
kusambaza huduma za Kifedha Vijijini ambako ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji
huduma hiyo.
IV: NISHATI NA MADINI
Mradi wa
Gesi
Mheshimiwa Spika, Kama ambavyo Wananchi wengi wanafahamu,
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) inaendelea kutekeleza
mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi Asilia katika maeneo ya Madimba,
Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa. Pia ujenzi wa Bomba la kusafirishia
Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mradi
huu utakapokamilika utaunganisha maeneo yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara,
Songo Songo, Kisiwani, Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo
la bahari ya kina kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi Asilia mbali
na matumizi mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa sasa Asilimia kubwa
unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na hivyo
kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.
Mheshimiwa
Spika, Katika utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika
hadi kufikia tarehe 30 Novemba, 2013:
Moja: Kukamilika kwa upakuaji
wa Shehena ya Sita (6) ya Mabomba ya Mradi yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169
katika Bandari ya Mtwara. Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013
ni 24,935 ya umbali wa kilomita 295.5;
Pili: Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari
Kilomita 498.5 zimekamilika;
Tatu: Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi
za kuhifadhia na kuyasambaza kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa kuchomelea.
Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9 yamekwishasafirishwa;
Nne: Uchimbaji wa
njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa Kilomita 27.0 umekamilika;
Tano: Uwekaji
wa mabomba kwenye njia yake sambamba na kuweka Mkongo wa Mawasiliano (Fiber Optic
Cable) umekamilika Kilomita 21.1; Sita: Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano.
Tayari Kilomita 7.30 za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano zimefukiwa; na
Saba: Utafiti
wa njia ya Bomba la Baharini nao umekamilika. Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona
niyataje.
Mheshimiwa Spika, Ni kweli kwamba kazi za mradi
huu ni kubwa lakini kwa ujumla zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo
za mradi huu ambazo tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi wa
Mradi ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi wa Gesi
na Mafuta. Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni za kitaalamu sana,
malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni kuajiri wafanyakazi Wakiwemo Wazawa
mapema ili waweze kushiriki na kujifunza kwa vitendo shughuli zote zinazohusiana
na ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi hatua kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa
ujenzi. Utaratibu huu utasaidia kupata wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha
(operations) na kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa
kipindi chote cha matumizi.
Mheshimiwa Spika, Vilevile
moja ya makubaliano katika Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu, Mkandarasi anawajibika
kuwapeleka Wafanyakazi kwenye mitambo na mabomba yanayofanya kazi kwa sasa kwa kipindi
kisichopungua mwezi mmoja ili wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli
zote za kuendesha mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya TPDC
ni kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa kipindi cha ujenzi
ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi wote wawe wamekwishapata uzoefu
wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, Kampuni nyingi zilizopo
Mtwara zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda vinavyohusiana
na matumizi ya Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa. Kwa mfano, Mpango
wa kujenga mitambo ya kutengeneza Gesi kuwa kimiminika (LNG) wa Kampuni ya British
Gas Tanzania utakuwa na utengenezaji wa ajira nyingi za kiwango kuanzia Kada
ya Chini na Kada ya Kati ambayo itasomesha Watanzania kupitia VETA katika fani mbalimbali.
Wako watakaosomeshwa katika fani ya Vyuma, wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu
na ufundi wa vyuma na umeme.
Katika Kada ya Kati, Kampuni
ya Gesi Tanzania wanatarajiwa kusomesha wataalamu 16,756 waliofaulu vizuri masomo
ya Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya 400,
na Watanzania wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta ni sawa
na Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo Nchini. Asilimia 30 iliyobaki ya watoa huduma
inatolewa na Wageni.
Katika Kada za Juu, Kampuni itasomesha
na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika kwenye Gesi na
Mafuta. Matokeo yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa VETA 370 wamesomeshwa
kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa na Wanafunzi 12 wa Kada
za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na Mafuta ndani na nje ya Nchi.
Mheshimiwa
Spika, Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya
British Gas Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa
na kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi kiasi hicho ni dhahiri kwamba ajira zitapatikana
kwa maelfu ya Watanzania. Katika hatua ya ujenzi, mradi utatoa ajira kwa maelfu; na
katika uzalishaji (operations) ajira nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini,
na katika mnyororo wa usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii
kuwapa Watanzania matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana, kuanzia
upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha
Wananchi wetu kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu. Ni fursa ya kipekee ambayo
Wananchi wetu wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.
V: MATUMIZI
YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)
Mheshimiwa Spika, Katika
mwaka wa fedha wa 2013/2014, Serikali ililiarifu Bunge lako Tukufu kuhusu mikakati
mbalimbali itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha
ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea kuimarisha matumizi
ya Mashine za Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devices- EFDs). Mashine
hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania
kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata mapato stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine
hizi zinasimamiwa kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa
moja kwenye Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.
Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka
huu, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi 200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia
Mashine za Kielektroniki. Walengwa wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara
kubwa zenye Mtaji wa kati ya Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika zoezi
hili, Wafanyabiashara Wadogo wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga
na wale wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata
kidogo.
Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa zoezi
hili kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa
Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na matumizi
ya Mashine hizi. Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu: Bei kubwa ya
ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za kutolea Risiti; Mchakato
uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa wa kutumia Mashine hizo; na
Gharama za matengenezo.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia
maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha
kwamba, Mashine za Kielektroniki zinafanya kazi zifuatazo:
Moja: Zinatoa
Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha
au kununua vitabu vingi vya kuandikia risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta
usumbufu;
Pili: Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi
na mali ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano;
Tatu: Mtumiaji
anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za mauzo yake kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa
mwaka na kwa wakati wowote kwa kipindi kisichopungua miaka mitano;
Nne: Humwezesha
Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za mauzo moja kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama
vile Taasisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;
Tano: Mashine
zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania, na kumtaarifu Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;
Sita: Kutuma
na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile Money”. Utaratibu huu unamwezesha Mtumiaji kutumia
Mashine hizi kulipia kodi na huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme,
Maji, Simu, n.k;
Nane: Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya Kiswahili
na Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;
Tisa: Mashine za Kielektroniki
zinaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na
hivyo kuweza kutoza Kodi halali.
Mheshimiwa Spika, Msingi
wa bei ya kununulia Mashine hizi za Kielektroniki umezingatia pamoja na mambo mengine,
manufaa na faida nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji na ubora wa mashine zenyewe. Aidha,
kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali
Duniani unaonesha kuwa mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo juu
zinauzwa na wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi Shilingi 778,377/=
(Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki za Nchi nyingine zinazotumia
mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani
360 hadi 870. Pamoja na bei hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana
na Wasambazaji wa Mashine hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.
Mheshimiwa
Spika, Kuhusu bei za karatasi za kutolea Risiti uchunguzi unaonesha
kuwa karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/= hadi Shilingi 4,500/= kuzingatia
ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo. Karatasi hizo zina uwezo wa kutoa wastani
wa risiti kati ya Risiti 200 hadi 1,000 kulingana na urefu wa “Paper Roll”! au Bunda.
Bei ya Karatasi hizi zinazojulikana kama “Thermal Paper” umezingatia kwamba ni za
kisasa na hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza
usalama.
Mheshimiwa Spika, Kuhusu utaratibu uliotumika
kuwapata Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji
wa karatasi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa ushindani
wa Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.
Mheshimiwa Spika, Katika kutafuta Watengenezaji na Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza Watengenezaji
Wanne (4) na Wasambazaji Sita (6) walipatikana kwa kutumia Zabuni ya wazi ya Kimataifa
(International Competitive Tendering) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi
wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009
mpaka Mei 2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji aliyechaguliwa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya “Memorandum of Understanding (MOU).
Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji wa utaratibu huohuo wa Zabuni ya Watengenezaji
ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News, The African, Tovuti ya TRA na Tovuti ya PPRA.
Jumla ya Wazabuni Kumi na Nne (14) walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja
baada ya saa Nne asubuhi tarehe 27 Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4)
walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano (5)
walipatikana kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi, huo ndio
utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na ushindani.
Mheshimiwa
Spika, Ili kuhakikisha ubora wa Mashine hizi za Kielektroniki,
Watengenezaji wametoa “Guarantee” ya muda wa miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika
bila kukusudia na watawajibika kutoa mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi
ya mashine hizo. Vilevile, kwa mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya Wasambazaji na
TRA, Wasambazaji wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika
ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda kuwahakikishia
Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia Mashine za Kielektroniki
haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu
za kila siku za biashara na kuwawezesha kulipa kodi stahiki Serikalini.
Mheshimiwa
Spika, Kwa kutambua umuhimu wa mashine hizi katika kuongeza Mapato
ya Ndani; na ili kuyashughulikia malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara yaliyojitokeza,
Serikali imesogeza mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine za Kielektroniki hadi tarehe
31 Desemba, 2013. Lengo ni kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa
kununua mashine hizi na kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana
na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi endelevu
na faida za Mashine za Kielektroniki kwa Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na
huduma. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote kushirikiana
na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu manufaa ya Mfumo huu wa
Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo
endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.
VI: USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa
Spika, Tarehe 16 - 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya kikazi Nchini
China kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Keqiang.
Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa
Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Viongozi wa Asasi za Sekta Binafsi Tanzania na
Watendaji Wakuu wa Serikali na Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo
na Wabia wetu kwa upande wa Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa
Spika, Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi ilihusu; kukuza mashirikiano
ya kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo na vyombo vya fedha ili kupata
mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili marafiki, kuona Sekta Binafsi ya Tanzania
inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa China na mwisho kutoa shukrani kwa misaada na
mikopo ambayo Nchi yetu imepokea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa
Spika, Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya Watu wa China ni miongoni
mwa Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na limepiga hatua kubwa sana katika
maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa yanayotokea katika Taifa la China, nilitoa
mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana na Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla
wake katika Nyanja za kiuchumi, utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano
ikiwa ni pamoja na soko kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.
Mheshimiwa
Spika, Katika ziara hiyo nilipata fursa ya kutembelea Miji ya Beijing,
Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata nafasi ya kukutana na Viongozi wa Makampuni
mbalimbali ya China. Kutokana na Mikutano hiyo, baadhi ya Makampuni na Taasisi za
Umma wameanza kuja Nchini kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na
Sekta Binafsi ili kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.
Mheshimiwa
Spika, Kwa ujumla ziara hii ilikuwa na mafanikio makubwa. Kwa mfano,
pamoja na kuendeleza na kudumisha ushirikiano ambao umeanzishwa na Viongozi waasisi
wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong
wa Jamhuri ya Watu wa China, kwenye ziara hiyo, niliweza kufanya mazungumzo na Waziri
Mkuu wa China Bwana Li Keqiang, pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China.
Ninaamini tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.
Mheshimiwa
Spika, Ziara yangu pia ilifanikisha kutiwa saini kwa Mikataba ya
ushirikiano wa Tanzania na China katika eneo la Sayansi na Teknolojia na katika Utalii.
Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu uuzaji wa bidhaa za baharini za Tanzania
Nchini China na kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao
la Pamba Nchini. Aidha, Mikataba ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na
Makazi baina ya Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya
Umeme - TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo - NDC na Shirika la Taifa la Nyumba
- NHC ilisainiwa.
Mheshimiwa Spika, Mafanikio
mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuyashawishi Makampuni makubwa ya usafiri wa anga
na Mawakala wa safari za kitalii kuwekeza Tanzania. Katika jitihada hizo nilikutana
na Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na China Travel
Service (Holdings) Hong Kong Limited. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa
kwa kiasi kikubwa Makampuni haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha utayari
wao wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na China. Aidha,
Kampuni ya China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited ambayo inafanya biashara
ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani wameonesha nia ya kuja kuwekeza
hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings
International Limited ambayo imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen
katika Jimbo la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali yetu
katika ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa Bagamoyo unaotarajiwa
kuwa “Trade Hub” ya Afrika.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
imedhamiria kuendeleza uchumi wake kwa lengo la kufikisha Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi
wa Kati kabla au ifikapo mwaka 2025. Viashiria vyote vinaonesha hivyo, na ndio sababu
Makampuni yote niliyozungumza nayo wakati wa ziara hiyo yameonesha shauku kubwa ya
kuja kuwekeza Tanzania katika Sekta mbalimbali na mengine tayari yapo Nchini kutekeleza
miradi mbalimbali. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kwa upande wake
tutajitahidi kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo tunayotarajia. Aidha,
tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na uwekezaji ili kuweza kuvutia Mitaji
na Wawekezaji wengi zaidi pamoja na Watalii kutoka China na maeneo mengine duniani.
VII: JUMUIYA
YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika, Mtakumbuka tarehe 7
Novemba, 2013 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania alihutubia Bunge ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la Jumuiya
ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda kulijulisha
Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 Kampala Nchini Uganda, Wakuu
wa Nchi hizo akiwemo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete walikutana na
waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki. Aidha,
Viongozi hao walizitaka Nchi Wanachama kukamilisha taratibu za kuridhia Itifaki hiyo
ifikapo mwezi Julai, 2014.
Mheshimiwa Spika,
Manufaa
ya Umoja wa Fedha ni pamoja na: kupunguza gharama ya kufanya biashara katika Nchi
Wanachama; kuwezesha Nchi Wanachama kuwa na kiwango kidogo na tulivu cha Mfumuko wa
Bei; kuwa na viwango vidogo vya riba ya kukopa; na kuepusha athari za ubadilishaji
wa fedha ndani ya Jumuiya kwa kuwa na Sarafu Moja. Matarajio ni kujenga ukanda tulivu
wa kifedha (Monetary and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na kusaidia ukuaji
wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.
Mheshimiwa Spika, Katika Mkutano huo wa Kampala Wakuu wa Nchi pia waliridhia Mfumo wa kuanzisha
Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuagiza kuwa ifikapo mwezi
Januari 2014, Nchi Wanachama ziwe zimeanza utekelezaji wake na kuukamilisha ifikapo
au kabla ya mwezi Juni 2014. Aidha, Wakuu wa Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo
ya Mpango Kazi wa kuelekea kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Walitumia
muda wa Mkutano huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na waliona kuna
umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.
Mheshimiwa
Spika, Kwa ujumla Mkutano huo ulikuwa na mafanikio sana hasa katika
kuimarisha Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu wa Nchi wote kwa pamoja walitumia muda huo
kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha kwamba mahusiano yetu kati ya Nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki yanadumu na tunaendelea kuijenga Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu
zetu zote.
X: PROGRAMU YA KUBORESHA MIJI NCHINI (URBAN LOCAL GOVERNMENT
STRENGTHENING PROGRAMME-ULGSP)
Mheshimiwa Spika, Wakati
wa kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge, nilieleza kuhusu Programu ya Kuboresha Miji
Nchini (Urban Local Government Strengthening Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5)
kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. Huu ni mwendelezo wa Programu ya Uendelezaji na Uboreshaji
Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities Programme-TSCP); ambao kwa sasa unakaribia
kumalizika utekelezaji wake. Programu hii ya ULGSP kwa sasa inahusisha Manispaa
11 na Miji 7. Manispaa hizo ni Tabora, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga, Musoma,
Songea, Singida, Iringa, Bukoba na Moshi. Miji mingine inayohusika ni Kibaha, Geita,
Babati, Korogwe, Mpanda, Njombe na Bariadi. Halmashauri hizi zinazojumuisha Manispaa
na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, ambavyo ni pamoja na:
Kuongeza Bajeti ya mapato kila mwaka; Kutokuwa na Hati Chafu za Hesabu
za Halmashauri, Kuunda Kamati za kushughulikia matatizo yanayotokana na Programu
kwenye ngazi ya Halmashauri, ngazi ya Kata na Mitaa; Kuhakikisha Programu hiyo
imetangazwa na kueleweka na wakazi wa Halmashauri za Manispaa na Miji; Kuhakikisha
kuna Wakuu wa Idara wa kutosha; Kuhakikisha Sheria za Manunuzi zinafuatwa; Kuhakikisha
Watu watakaohamishwa na Programu na kulipwa fidia hawazidi nyumba 20; Kuhakikisha
miradi iliyotekelezwa inalingana na thamani ya fedha iliyotumika; Kutekeleza miradi
ya miundombinu iliyoko kwenye menu; Kupeleka taarifa za kila robo mwaka za miradi
kwa muda unaotakiwa; Kuhakikisha kuna Master Plan ya Mji; Kuhakikisha ukusanyaji
wa kodi ya majengo unaongezeka kati ya Asilimia 5 hadi 30; na Kuhakikisha taarifa
za Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye vikao vya Halmashauri kila robo mwaka.
Ukikosa
hapa fedha hizo hazipatikani. Mheshimiwa Spika, Nimetaja baadhi
ya Vigezo kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila Sekta ya Halmashauri. Upimaji wa
vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa mwaka; na Halmashauri zitakazoshindwa kufikia
Alama (Marks) 60 na kuendelea, watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na
Mabaraza ya Madiwani lazima yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na kutekelezwa
kikamilifu. Aidha, TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria wale wote watakaozembea
katika kutimiza vigezo hivi na kuathiri maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa
Spika, Programu hii ambayo ni ya kwanza Afrika itatumia Dola za
Kimarekani 255, fedha ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai mwaka huu, lakini kutokana
na matatizo ya ubadhirifu yaliyojitokeza kwa Wasimamiaji wa fedha zilichelewa kutolewa.
Hata hivyo, baada ya kuwapeleka wahusika wa ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria, Wafadhili
waliridhika na hatua zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013 Wafadhili walitoa
fedha za Awamu ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri hizo 18. Miradi iliyopo
kwenye Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na mifereji ya mvua,
uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi, upimaji viwanja, utengenezaji
wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka na uboreshaji wa makazi. Hii ni baadhi
ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa na Halmashauri zenyewe kufuatana na matatizo ya Miji
hiyo. Hivyo, ninawaomba TAMISEMI - wasimamie Programu hii vizuri ili Miradi husika
iweze kutatua matatizo ya Wananchi katika maeneo yao na kuhakikisha Mapato ya Halmashauri
yanaongezeka. Lengo ni kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya Miradi hiyo
kukamilika.
XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA
SERIKALI ZA MITAA
Mheshimiwa Spika, Kama ambavyo itakumbukwa,
wakati wa majadiliano ya Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu
zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa, kwa mwaka 2011/2012, Waheshimiwa Wabunge walionesha
masikitiko yao kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na baadhi ya Halmashauri
Nchini. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia mjadala huo walidai kuwa Serikali
imekuwa haichukui hatua dhidi ya Watumishi wanaofanya makosa katika Halmashauri. Napenda
kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na matatizo na changamoto mbalimbali
zilizopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha
za Umma, Serikali imejitahidi kuimarisha usimamizi na utendaji katika eneo hili. Jitihada
hizi zimedhihirishwa na Matokeo ya Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ambayo yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi zinazotolewa kwa
Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000 hadi sasa. Kwa mfano, mwaka
2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha kuwa Halmashauri zilizopata Hati safi zilikuwa
16 sawa na Asilimia 14 ya Halmashauri zote. Aidha, Idadi ya Halmashauri zilizopata
Hati zenye Shaka zilikuwa 23, sawa na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati Chafu
zilikuwa 75 sawa na Asilimia 65 ya Halmashauri zote.
Mwaka 2005/2006
Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati Safi iliongezeka hadi kufikia 53, sawa na Asilimia
43 na Halmashauri zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na
Halmashauri zenye Hati Chafu zilikuwa Nne (4), sawa na Asilimia Tatu (3).
Mwaka
2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi ambapo Halmashauri zilizopata Hati
Safi ziliongezeka maradufu hadi kufikia 104, sawa na Asilimia 78 na zilizopata Hati
zenye Shaka zilikuwa 29, sawa na Asilimia 21 na hakukuwa na Halmashauri iliyopata
Hati Chafu.
Mheshimiwa Spika, Jitihada hizi ni kubwa. Hivyo,
Serikali itaendelea kuimarisha Usimamizi na Udhibiti na Mapato na Matumizi ya Serikali
katika Sekta zote na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi na tija katika
utendaji na kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo ni kuongeza kasi
ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi kwa haraka.
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na jitihada hizo za Serikali zinazoonekana, napenda
kuwahakikishia kwamba Watumishi waliohusika na ubadhirifu wa mali na fedha za Umma
wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo, na kufikishwa
mahakamani. Aidha, kesi za Watumishi hao ziko katika Mahakamani na katika Vyombo
vya nidhamu vya Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao kuhakikisha
kwamba tunajenga nidhamu. Kutokana na hatua hizo kati ya mwaka 2011/2012 hadi Septemba,
2013 jumla ya Wakurugenzi 52, Wakuu wa Idara 65 na Watumishi wengine 749 wamechukuliwa
hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri mbalimbali
Nchini. Hatua hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:
Waliofukuzwa
kazi ni 232, Waliosimamishwa kazi ni 186, Waliovuliwa Madaraka ni 33, Waliopunguziwa
Mshahara ni 1, Walioshushwa Cheo ni 32, Walipewa ONYO ni 113, Waliofikishwa
Mahakamani ni 233, Waliofikishwa Polisi na TAKUKURU ni 36.
Serikali
itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha fedha za Umma zinatumika vizuri.
Mheshimiwa
Spika, Pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi
hao mmoja mmoja, Serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana
na tatizo la ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri. Juhudi hizo ni pamoja
na kuongeza uwezo kwa kuajiri Wahasibu wa kutosha katika Halmashauri zetu; kuanzisha
Kamati za Mapato na Matumizi katika ngazi zote za Halmashauri na kutoa mafunzo ya
mara kwa mara kwa Kamati za Mapato na Matumizi za Halmashauri zote. Mbinu nyingine
zinazotumika ni kufanya Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na ubadhirifu wowote uliojitokeza.
Kwa mfano, Katika mwaka wa fedha 2011/12 kumefanyika Kaguzi maalumu kwenye Mamlaka
za Serikali za Mitaa kumi na nne (14), ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa,
Musoma, Kilwa, Temeke, Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda.
Kaguzi hizo zimesaidia sana katika kujenga nidhamu ya Watumishi katika Halmashauri
hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeweza kubadili
na kuweka Mfumo wa ‘Lawson’ katika kila Halmashauri ili kumaliza tatizo la Mishahara
kwa Watumishi waliofariki, walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile kuna Mfumo wa Epicor
9.05 ambao zinasaidia kudhibiti Bajeti za Mapato na Matumizi katika Halmashauri Nchini.
Mafunzo kuhusu matumizi ya Mifumo hii mipya yanaendelea kutolewa ili kuweza kutumia
mifumo hii kwa ufanisi. Vilevile, Wakuu wa Mikoa walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao
vya Baraza za Halmashauri; katika kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo
hazikupata majibu kikamilifu, Sheria zifuatwe na wenye kuhusika na ubadhirifu wowote
wachukuliwe hatua zinazostahili. Aidha, Maafisa Masuuli (Wakurugenzi) wanaohusika
na Hoja mbalimbali za Ukaguzi wanapaswa kuitwa kwenye Halmashauri walizotoka ili kujibu
hoja zinazowahusu bila kujali wamehamishiwa wapi.
XI: HITIMISHO Mheshimiwa
Spika, Tumekuwa na muda mzuri wa kujadili masuala muhimu yanayohusu
maendeleo ya Nchi yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu tulichokuwa katika Mkutano huu.
Napenda niwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru
wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti
wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza Vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru
tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu
wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake
ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali
za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya
kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia
Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama
Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki
katika Mkutano huu.
Niwashukuru Wabunge wote kwa kujadili
vizuri hoja za zilizojitokeza hapa Bungeni. Lakini kipekee niwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri Wanne waliokubali kubeba jukumu ka kuwajibika kwa yote yaliyotokea. Tunawashukuru
kwa uzalendo wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila la kheri katika maisha yao.
Mheshimiwa
Spika, Tunahitimisha shughuli za Bunge hili tukiwa tumebakiza siku
chache kabla ya kufika Mwisho wa Mwaka huu 2013. Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye
wingi wa Rehema atujalie katika siku hizi chache tuweze kusherehekea Sikukuu njema
ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa mwaka na kuingia Mwaka Mpya 2014 kwa Amani na
Furaha!.
Mheshimiwa Spika, Kama ambavyo Waheshimiwa
Wabunge wote tunavyofahamu, tutakuwa na Bunge la Katiba litakalofanyika mapema mwakani
na kwa tarehe itakavyopangwa. Kutokana na utaratibu huo ni dhahiri kwamba wengi wetu
tutakutana wakati wa Bunge la Katiba. Nitumie fursa hii kuwatakia safari njema mnaporejea
kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Krismas na
Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa
Spika, Baada ya kusema hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liahirishwe
hadi litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na Tano wa Bunge la Bajeti tarehe 06
Mei, 2014 saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu hapa Dodoma.