AMECEA yasikitishwa na kuzuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA limepokea
kwa masikitiko makubwa machafuko ya kisiasa na kijamii yanayoendelea nchini Sudan
ya Kusini na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu. Ni matumaini ya AMECEA kwamba,
hali hii itaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka, ili haki, amani, upendo na mshikamano
viendelee kutawala miongoni mwa wananchi wa Sudan ya Kusini.
Inasikitisha kuona
kwamba, baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kutawala nchini Sudan kwa miaka arobaini
na hatimaye, kura ya maoni ikapigwa na Sudan ya Kusini ikapewa uhuru kamili wa kujiamlia
mambo yake, imerudi tena katika vita ya wenyewe kwa wenyewe! Mwaka mmoja wa uhuru
wa Sudan ya Kusini, unapaswa kuwa ni kipindi cha kujijenga na kujiimarisha katika
mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na kuweka mikakati ya maendeleo endelevu kwa ajili
ya ustawi wa wananchi wa Sudan ya Kusini na wala si kujikita katika vita!
Ni
maneno ya Askofu mkuu Tarcisius Zizaye, Rais wa AMECEA wakati huu Jumuiya ya Kimataifa
inapoyaelekeza macho yake Kusini mwa Sudan. AMECEA inaendelea kutolea sala zake, ili
amani na upatanisho viweze kupatikana tena Sudan ya Kusini.