2013-12-20 09:29:54

Watu wanakimbia nchi yao kama ilivyokuwa wakati wa Yesu!


Kinzani na mapambano ya kutafuta mali na madaraka; ukosefu wa heshima na utu wa binadamu; watu kushindwa kuzingatia utawala wa sheria; malumbano yalisyokuwa na tija wala mashiko; kumong'onyoka kwa maadili na utu wema; kuporomoka kwa mila na desturi njema miongoni mwa wananchi wa Haiti; rushwa na ufisadi; hali ya kutovumiliana wala kuthaminiana na mapambano kati ya matajiri na akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi ni kati ya mambo yanayohatarisha amani na usalama wa wananchi wa Haiti katika ujumla wao.

Hivi ndivyo wanavyoandika Maaskofu Katoliki kutoka Haiti katika ujumbe wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2013. Vita, kinzani za kisiasa, kijamii na kidini sehemu mbali mbali za dunia kwa kiasi kikubwa ni hali inayofanana kabisa na mahali alipozaliwa Yesu Kristo. Kinzani na malumbano yasiyokuwa na tija yanaendelea kuhatarisha mustakabali wa maisha ya wananchi wa Haiti, kiasi kwamba, wanashindwa kuishi kwa pamoja kama ndugu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linasema kwamba, hata Yesu alikumbana na "majanga" katika maisha, akatishiwa kifo hata katika utoto wake, jambo ambalo liliwalazimu wazazi wake kukimbilia Misri ili kumhifadhi Mtoto Yesu. Hii ndiyo hali halisi ilivyo nchini Haiti, kuna makundi makubwa ya wananchi wa Haiti yanaikimbia nchi yao kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao baharini. Watu hawana woga tena wa kukabiliana na hali ngumu ya maisha ugenini kwani wamechoka kuwaona viongozi ambao wanashindwa kutekeleza dhamana na wajibu kwa raia wao.

Katika mchakato wa kutafuta maisha bora zaidi, kwa bahati mbaya wanakumbana na nyanyaso, dhuluma, ubaguzi na wakati mwingine kifo kinawaondosha mara moja kama ndoto ya mchana! Maaskofu wanajiuliza ni nani ambaye anaweza kulifahamu fika Fumbo la Msalaba linalowakabili wananchi wa Haiti hata wakiwa ndani ya nchi yao? Ni nani ambaye anawajibu wa kuhakikisha kwamba, wananchi wa Haiti wanakuwa na leo pamoja na kesho iliyo bora zaidi?

Ni nani atakayewasaidia kuanza tena mchakato wa kuifufua nchi yao iliyoharibiwa vibaya kwa tetemeko la ardhi? Maaskofu wanasema, huu ni wajibu wa wananchi wote wa Haiti katika ujumla wao, wakisaidiwa na wadau pamoja na wapenda maendeleo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Nchi ya Haiti inataka kuona kila mwananchi akishiriki kikamilifu katika ujenzi wa nchi yake kwa njia ya umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa.

Wananchi wanapaswa kujikita katika majadiliano ya kweli ili kutafuta mafao ya wengi sanjari na kuhakikisha kwamba, kinzani na migogoro ya kijamii inapatiwa ufumbuzi wa kudumu, ili wananchi waweze kujenga tena mshikamano wa dhati miongoni mwao!







All the contents on this site are copyrighted ©.