2013-12-20 07:45:18

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 1V ya Kipindi cha Majilio


Hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutujalia tena siku nzuri kama hii na hasa tunapoijongea meza ya Neno lake. RealAudioMP3

Ni Dominika ya IV ya Kipindi cha Majilio, tukikaribia kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, Mfalme wa amani, Mtoto Emanueli. Katika somo la kwanza tunapata kusikia kuwa Mungu atatoa ishara na hapa ndipo kuna mzizi na kiini cha masomo ya Dominika hii. Basi ishara yenyewe ni Mtoto Emanueli yaani Mungu pamoja nasi.

Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, katika somo la kwanza tunakutana na Mfalme Ahaz ambaye alikuwa wa ukoo wa Daudi. Wote twatambua kuwa toka ukoo wa Daudi angezaliwa Masiha mkombozi, kadiri ya ahadi ya Mungu. Pamoja na ahadi hiyo mfalme Ahaz hakuwa mtu wa dini, kumbe hakuweka tumaini lake katika ahadi za Mungu. Katika utawala wake kwa sababu ya kukosa tumaini katika ahadi za Mungu atapoteza madaraka na kuliweka taifa la Yuda katika taabu.

Inajulikana baada ya kutishiwa kutekwa taifa lake, anakimbilia kuomba msaada kwa Siria na hapa ndipo kuna kuibuka kwa nabii Isaya akikemea jambo hilo na kumwambia aombe na kutumainia hadi za Mungu kwa taifa la Yuda.

Hata hivyo Ahaz hatasikiliza ushauri huo. Kwa kukataa ushauri huo basi nabii Isaya, atamwambia omba ishara toka kwa Mungu kama huamini! Ahaz anaendelea na kiburi chake na anasema siombi ishara yoyote. Hapa kunatokea kutekwa na kuingia katika mateso makubwa, maana hao Wasiria aliowategemea walimgeuka na kuanza kumtawala wao wenyewe baada ya kumsaidia kushinda vita! Mara kadhaa nasi hatuko mbali na Ahaz, hasa tunapokomaa katika kiburi chetu cha kutowasikiliza manabii wa leo!

Mpendwa, nabii Isaya akitambua yatakayotokea yaani vita na kutawaliwa kama nilivyokwishasema, anasema pamoja na kwamba umekataa, Mungu atatoa ishara na ishara ndo hii “tazama bikira atapata mimba, atazaa mtoto wa kiume na atamwita Emanueli”. Huyu bikira anayetajwa ni mke mdogo wa Ahaz ambaye atamzaa Hezekia, ambaye atatawala kwa mafanikio lakini, bado kile ambacho kinaaguliwa yaani Emanueli hakikamiliki katika Hezekia kwa maana kutakuwa na mapungufu!

Ndiyo kusema, mama huyu bikira atakuwa Maria Mama wa Mungu atakayemzaa Yesu Kristu, Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Katika Bikira huyu na katika Emanueli Kristu kuna ukamilifu wote. Hii ndiyo ishara yetu, ndiyo amani yetu na ukombozi wa taifa letu.

Mpendwa msikilizaji, kumpokea Emanueli, Mungu pamoja nasi, yafaa kutanganza Injili kwa unyenyekevu na kwa furaha. Ni kwa jinsi hiyo tutaweza kuwajengea watu wa Mungu furaha na tumaini la ukombozi wa milele kama atuambiavyo Mt Paulo katika somo la II. Mpendwa mwana wa Mungu katika somo la Injili tunapata kusikia kuzaliwa kwa Mtoto Emanueli, Mwana wa Mungu. Anazaliwa katika ukoo wa Daudi katika familia ya Yosefu mfanyakazi. Ni ukamilifu wa ile ishara tuliyoisikia katika somo la kwanza.

Anazaliwa kwa uwezo wa Mungu na hivi Yosefu mtu mwema anapokea habari ya kuwa mchumba wake, atamzaa Mwana wa Mungu na katika hali ya kiutu angeweza kukataa kwa maana hakumjua mke wake. Hata hivyo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na katika unyoofu wake, Mtakatifu Yosefu anakubali jukumu takatifu la kuwa Baba mlishi. Mtakatifu Yosefu hajengi mashaka kama ya Yohane Mbatizaji bali anagonga mara moja kiini cha habari njema yakwamba katika ukoo wa Daudi atazaliwa Masiha. Anapata mara moja jukumu la kumpatia jina mtoto huyu, yaani Yesu.

Mpendwa msikilizaji, kama nilivyokwishasema ishara ni Kristu mwenyewe katika maisha yetu kumbe hatuna haja ya kutafuta ishara nyingine. Jambo la msingi ni kuangalia anataka nini katika maisha yetu, anataka kazi yangu ninayoifanya ifikishe Injili ya upendo, injili ya uhai wapi? Maisha yangu ya ndani yanamwelekea Masiha au ni maisha ya juujuu tu!! Je ninajiweka tayari kufunua moyo wangu kwa ajili ya fumbo la Noeli kama Mama Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walivyokuwa watu wa kwanza kufungua mioyo yao kwa ajili ya Mungu? Tukijiweka katika nafasi ya Watakatifu hawa wawili tutaweza kusherehekea kwa uhakika na kwa furaha Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu.

Tukumbuke pia matatizo ya ulimwengu wa kiuchumi na kisiasa yaweza kuzuia furaha na kuanza kujiuliza hivi Mungu aweza kuruhusu mambo hayo? Basi mara moja kumbuka kiburi cha Ahaz kuhusu ishara na tumaini kwa Mungu. Ndiyo kusema, kiburi hichohicho kinaendelea katika ulimwengu wetu wa leo, lakini bado Mungu anatujia na kutupatia ishara ya wokovu yaani amani. Ndiyo kusema tukazanie maisha ya sala na upendo kwake yeye na kwa watu wa Mungu kwa ajili ya kuondoa giza linalotuzunguka.

Mpendwa msikilizaji, kuweza kuondoa kiburi lazima kuwa tayari kumwachia Mungu maisha yetu kama ambavyo Mtakatifu Yosefu anakubali kumwachia Mungu mchumba wake Mama Bikira Maria awe daraja la kutuletea ukombozi. Kama ndivyo, basi tuombe neema ya Mungu kwa njia ya Watakatifu hawa tuweze kuwa tayari kwa yote yatokayo kwa Mungu.
Nikutakie Dominika ya IV njema na Noeli njema ukiimba nyimbo zuri na za kumsifu Mungu kwa ajili ya zawadi ya amani duniani. Tumsifu Yesu Kristo na Bikira Maria.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.