Fumbo la Umwilisho linagusa: maskini, uinjilishaji na furaha!
Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa katika mahubiri yake ya tatu
wakati huu wa Kipindi cha Majilio, amegusia kuhusu Fumbo la Umwilisho mintarafu tafakari
iliyofanywa na Mtakatifu Francisko wa Assisi; uhusiano kati ya maskini na Siku kuu
ya Noeli; changamoto ya kuwapenda, kuwasaidia na kuwainjilisha maskini. Siku kuu ya
Noeli iwe ni kielelezo cha furaha mbinguni na amani duniani.
Mahubiri haya
yamehudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu na wakuu wa Mashirika
ya Kitawa na Kazi za Kitume. Padre Cantalamessa anasema kwamba, utamaduni wa kutengeneza
Pango la Mtoto Yesu umeasisiwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyependa kuwaonjesha
waamini umaskini ambayo Mtoto Yesu alikumbana nao wakati wa kuzaliwa kwake mjini Bethelehemu:
Huyu ndiye Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu akawa mwanadamu; akajinyenyekesha
hata kufa Msalabani; Ni Mungu aliyeonja umaskini wa binadamu.
Kadiri ya Mafundisho
ya Mababa wa Kanisa, kuna uhusiano mkubwa kati ya Siku kuu ya Noeli na Maskini wanaonesha
unyenyekevu na mateso, kiasi hata cha Yesu mwenyewe kujitambulisha nao! Mwaliko kwa
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwahudumia maskini kwa njia ya matendo ya
huruma, kwani kwa kufanya hivi kwa maskini na wadogo, wanamhudumia Kristo mwenyewe!
Kanisa halina budi kujitambulisha na Maskini kama alivyowahi kusema Papa Yohane XXIII,
wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Hii ni kutokana
na ukweli kwamba, kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo, wanakufa na kufufuka pamoja na
Kristo. Waamini na watu wenye mapenzi mema, waguswe na mateso pamoja na mahangaiko
ya maskini duniani na kamwe wasiwapatie kisogo. Jamii ijitahidi kujenga na kuimarisha
utamaduni wa Injili ya Upendo na Maisha kwa kuwasaidia: wazee, maskini na watoto wanaokumbana
na baa la njaa na utapiamlo ili waweze kuwa na uhakika wa maisha ya leo na kesho iliyo
bora zaidi kwa kubadili mtindo wa maisha!
Padre Cantalamessa anasema, upendo
kwa maskini ni kielelezo cha utakatifu wa maisha kama walivyoonesha watakatifu wengi,
kati yao Mtakatifu Vincenti wa Paulo na Mama Theresa wa Calcutta. Utakatifu umekuwa
ni njia na karama ya maisha yao ya kitawa.
Maskini waheshimiwe na kuthaminiwa
kama binadamu na ndugu zake Yesu, kwani, udugu ni msingi na njia ya amani. Maskini
wasaidiwe kupambana na majanga ya maisha kwa njia ya mshikamano wa upendo unaoongozwa
na kanuni auni. Kamwe, watu wasizibe maskio kwa kutotaka kusikiliza kilio cha maskini.
Jumuiya ya kimataifa iunganishe nguvu zake katika mapambano dhidi ya baa la umaskini
wa hali na kipato.
Maskini pia wanapaswa kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu!
Washirikishwe Neno la Uzima na Mkate ulioshuka kutoka mbinguni; waonjeshwe tone la
matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Maskini wana haki ya kusikia ujumbe mzima
wa Injili ukitangazwa kwao.
Kwa Mtakatifu Francisko, Siku kuu ya Noeli ilikuwa
ni kielelezo cha kuonesha ile furaha inayobubujika kutoka katika undani wa moyo wa
mwamini kwani Mtoto Yesu anakuja kati ya watu wake katika hali ya umaskini, kielelezo
cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Nyimbo za Noeli zinawaonjesha
waamini na watu wenye mapenzi mema furaha ya Noeli.