Wakristo na uhuru wa kidini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza semina ya siku moja
iliyoandaliwa na Mradi wa uhuru wa kidini kutoka Chuo Kikuu cha Georgetwon pamoja
na Kituo cha Masuala ya Kidini cha Berkley, vyote kutoka nchini Marekani. Askofu mkuu
Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa
mjini Vatican alishiriki katika warsha hii.
Anasema, dhana
ya uhuru wa kidini ni jambo ambalo limeibuliwa na Kanisa na kushuhudiwa na waamini
kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama alivyofanya
Mtakatifu Thomas More. Waamini kwa kusukumwa na dhamiri nyofu na akili timamu wanayo
haki ya kukataa utawala wa kidhalimu na nyanyaso za kidini. Dhana hii imefundishwa
na Yesu mwenyewe na Mtakatifu Paulo anasema, waamini wamekombolewa na Kristo na kwamba,
uhuru wa ndani unayo nafasi ya pekee hata katika maisha ya hadhara ndani ya Jamii.
Jumuiya
ya Kimataifa Mwaka 2013 inaadhimisha Miaka 1700 tangu Azimio la Milano lilipopitishwa
na hivyo kutoa haki ya kuwa na uhuru wa mtu kuabudu dini anayotaka. Uhuru wa kidini
ni chimbuko la tamaduni na urithi mkubwa wa maisha ya binadamu, mahusiano na mshikamano
kati ya watu wa mataifa na dini mbali mbali. Uhuru wa kidini ni dhana inayopaswa kuangaliwa
kwa makini kwani inaweza kutasiriwa kinyume chake.
Hii ni dhana ambayo inapaswa
kutekelezwa kwa kuzingatia akili na imani; kinyume kabisa cha utepetevu wa imani na
maisha ya kiroho; misimamo mikali ya kiimani na kidini; kwani kwa makundi kama haya,
uhuru wa kidini unaonekana kutishia mawazo na misimamo yao, mambo yanayohatarisha
amani na utulivu duniani.
Askofu mkuu Dominique Mamberti anasema, Mababa wa
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipokuwa wanakazia uhuru wa kidini si kwmaba, walikuwa
wanaleta Mafundisho mapya ndani ya Kanisa, bali walipenda kupyaisha mang’amuzi ya
wengi katika maisha ya binadamu yanayosaidiwa na akili na utashi; mambo msingi yanayomwajibisha
binadamu katika utekelezaji wa maamuzi yake msingi.
Mwanadamu kisimngi anasukumwa
kutafuta asili na ukweli mkamilifu, ambao ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, kiini cha utendaji
wa akili ya mwanadamu na chemchemi ya uhuru. Mwingiliano wa mambo yote haya unamwezesha
mtu kutambua na hatimaye, kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu.