Mwenyezi Mungu anaweza kumkirimia mwanadamu upya wa maisha hata katika Jangwa na Ugumba!
Unyenyekevu ni fadhila muhimu sana inayomwezesha Mwenyezi Mungu kushirikiana na binadamu
katika kutekeleza mipango na malengo yake. Kwa njia ya unyenyekevu, Mwenyezi Mungu
anaweza kufanya mambo ya ajabu hata pale ambapo mwanadamu alikwisha hesabika kuwa
ni tasa na hawezi kuzaa tena.
Huruma na upendo wa Mungu unajionesha kwa namna
ya pekee kwa wanawake tasa ambao kwa njia ya unyenyekevu wa maisha yao, Mwenyezi Mungu
ameweza kuwainua kutoka mavumbini kama ilivyojionesha kwa Elizabeth, Mama yake Yohane
Mbatizaji anayesimuliwa wakati huu wa Kipindi cha Majilio.
Hii ni sehemu ya
mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 19 Desemba 2013
kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Wanawake wagumba waliokuwa
wamekata tamaa, wanaonja matumaini mapya kwa njia ya unyenyekevu mbele ya Mwenyezi
Mungu.
Hii inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote anaweza kuchipusha
maisha mapya hata kwenye "Jangwa" la maisha ya mwanadamu na kwamba, Mwenyezi Mungu
daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kwa njia ya ukombozi, anasema
Baba Mtakatifu, Mwenyezi Mungu anamkirimia mwanadamu maisha, lakini jambo la msingi
ni kuhakikisha kwamba, binadamu anashirikiana na Mungu katika utekelezaji wa mipango
na mikakati yake.
Mwenyezi Mungu anampatia mwamini neema na baraka za kuweza
kutembea katika hija ya utakatifu wa maisha. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu
kwa waamini kuomba neema na baraka hizi kwa kutambua mapungufu yao ya kibinadamu,
ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu, hata katika majanga ya maisha.
Waamini
wanakumbushwa kwamba, kiburi ni chukizo mbele ya Mungu. Kipindi hiki cha Majilio,
kiwawezeshe waamini kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka
nyingi anazowakirimia katika maisha yao