Wasi wasi unazidi kuongezeka Afrika Magharibi kutokana na kinzani na migogoro ya kijamii
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi linalounganisha Maaskofu
kutoka: Senegal, Mauritania, Cape Verde na Guinea Bissau, hivi karibuni limeonesha
wasi wasi wake kutokana na kinzani, vurugu na vita inayoendelea katika baadhi ya nchi
jirani. Maaskofu katika mkutano wao uliofanyika mjini Ziguinchor, Senegal, eneo lililotaka
kujitenga na Senegal kunako mwaka 1982.
Maaskofu wamesali
kwa ajili ya kuombea haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa na kuzitaka Serikali
zao, kuhakikisha kwamba, zinajenga mazingira yatakayowezesha wananchi kuishi kwa amani
na utulivu. Maaskofu wanawaalika vijana kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi
za binadamu na kamwe wasitumiwe na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kusababisha vita
na machafuko kati ya watu.
Maaskofu wanasema wataendelea kushirikiana na viongozi
wa kidini na wanasiasa wanaotaka kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi
na maendeleo ya wote. Ni mwaliko wa kukusanya nguvu za wananchi ili kulinda amani
ambayo ni kielelezo na jina jipya la maendeleo endelevu.
Mkutano huu umehudhuriwa
pia na Askofu mkuu Luis Mariano Montermayor, Balozi wa Vatican nchini Mauritania ambaye
amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama nyenzo muhimu sana ya
kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Wamekazia ujenzi wa umoja na mshikamano
miongoni mwa vyuo vikuu vya Kikatoliki katika eneo hili.