2013-12-18 11:23:22

Mwilisheni huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi!


Noeli ni Siku kuu ambayo Mama Kanisa anakumbuka kwa namna ya pekee Fumbo la Umwilisho. Huduma ya upendo na mshikamano wa dhati ni sehemu ya mchakato wa kumwilisha uwepo wa Mungu katika uhalisia wa maisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hawa ndio: maskini, wagonjwa, wazee na vilema; wafungwa na wakimbizi.

Huu ni ujumbe uliotolewa na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem, Jumanne, tarehe 17 Desemba 2013 alipokuwa anawashukuru wafanyakazi wa Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza dhamana hii nyeti nchi Takatifu. Anasema, Noeli ni Fumbo la Umwilisho wa Upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi.

Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mshikamano kati ya Mungu na binadamu, changamoto ya kumwilisha upendo huu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Noeli ni kielelezo cha umoja kati ya Mungu na binadamu, mwaliko wa kuendeleza mshikamano huu kati ya binadamu kwa kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema anasema Patriaki Twal wajenge na kuimarisha mshikamano katika hatua na medani mbali mbali za maisha na kwamba, Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotekelezwa na Shirika la Misaada la Kanisa huko Nchi Takatifu na Yordani, kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi wanaotafuta hifadhi ya maisha yao katika maeneo salama. Hawa ni wakimbizi wanaotoka Iraq, Syria na Misri.







All the contents on this site are copyrighted ©.