2013-12-18 09:43:39

Mwenyeheri Pietro Favre kutangazwa kuwa Mtakatifu


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililotolewa na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, ili Mwenyeheri Pietro Favre, Padre Myesuit aweze kutangazwa kuwa ni Mtakatifu.

Padre Favre alizaliwa tarehe 13 Aprili 1506 huko Le Villaret, Ufaransa, akafariki dunia mjini Roma, tarehe Mosi Agosti 1546.

Baba Mtakatifu ameridhia miujiza inayosadikiwa kutendwa kwa maombezi ya watumishi wa Mungu wafuatao: Sr. Maria Teresa Demjanovich, mtawa wa Shirika la Upendo la Mtakatifu Elizabeth, aliyezaliwa tarehe 26 Machi 1901 huko Bayonne, nchini Marekani na kufariki dunia tarehe 8 Mei 1927.

Kanisa limetambua pia karama za kishujaa zilizooneshwa na Mtumishi wa Mungu Padre Emmanuele Herranz Estables, Mwanzilishi wa Shirika la kitawa la Bikira Maria Mama wa Mateso. Yeye alizaliwa tarehe Mosi, Januari 1880, huko Campillo de Duenas, Hispania na kufariki dunia tarehe 29 Juni 1968 huko Madrid, Hispania.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia karama za kishujaa zilizooneshwa na kushuhudiwa na Mtumishi wa Mungu Giorgio Ciesielski, mwamini mlei na Baba wa familia. Alizaliwa tarehe 2 Februari 1929 na kufariki dunia hapo tarehe 9 Oktoba 1970.







All the contents on this site are copyrighted ©.