Ndani ya Kanisa waamini wanapaswa kujifunza kwamba Huduma ya Kiinjili haipaswi kumezwa
na utukufu wala mafao ya mtu binafsi. Haya ni kati ya mafundisho makuu yanayotolewa
na Baba Mtakatifu Francisko na kujionesha kwa namna ya pekee katika ujumbe aliouandika
kwa Padre Fray Josè Narlaly, Mkuu wa Shirika la Fumbo la Utatu Mtakatifu, linaloadhimisha
Kumbu kumbu ya miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Juan de Mata na miaka 400
tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Batista wa Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya
asili, kiongozi aliyeleta mageuzi makubwa ndani ya Shirika hili.
Baba Mtakatifu
anasema, watakatifu hawa hata kama walibahatika kwa namna ya pekee kuwa na maisha
yenye heshima, utulivu na uhakika wa usalama, walipokea wito maalum kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, aliyewachangamotisha kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu anasema, watakatifu hawa
ni mfano bora wa kuigwa, kwani walikubali kupokea changamoto zilizojitokeza katika
maisha yao na Kanisa linapowasherehekea wakati huu ni kwa sababu walijitosa kwa namna
ya pekee, kupokea na kuubeba Msalaba wa Kristo katika hali ya unyenyekevu, wakajiachilia
mikononi mwa Mungu bila kumwekea masharti wala vizingiti, ili aweze kutekeleza kazi
miongoni mwa watu wake.
Kama ilivyokuwa kwa watakatifu hawa, waamini wote
wanaalikwa kwa namna ya pekee kuonja ile furaha inayobubujika kwa kukutana na Yesu
ili kuvuka vikwazo vya ubinafsi, raha na starehe, tayari kuwaendelea wote wanaohitaji
kuona tena Mwanga wa Injili. Kwa miaka mingi Shirika la Fumbo la Utatu Mtakatifu,
limekuwa ni maskani ya maskini; mahali ambapo watu waliojeruhiwa kiroho na kimwili
wanagangwa kwa njia ya sala na huduma inayojikiza katika huruma na upendo.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema, Shirika la Fumbo la Utatu Mtakatifu ni mfano bora wa
kuigwa kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma, changamoto ya kujiondoa
katika kishawishi cha mtu kujitafuta mwenyewe wala kugubikwa na uroho wa mali na madaraka.
Viongozi na waamini wajifunze kushirikishana karama na vipaji walivyopokea
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, wanaalikwa kuwa ni wasimamizi bora
na kwa ajili ya huduma kwa maskini ambao idadi yao inazidi kuongezeka siku hadi siku,
kiasi kwamba, Kanisa haliwezi kuwafumbia macho kana kwamba, hawapo, bali wanapaswa
kuonjeshwa huduma ya huruma na upendo.
Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe
wake kwa Shirika la Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kuwasihi kumkumbuka katika sala na
maombi yao katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, bila kuwasahau
maskini, kwani wao kwa upande wao kamwe hawawezi kumsahau, kama alivyofanya Yesu Mwenyewe,
kwa kuwapatia hifadhi katika sakafu ya moyo na utume wake hapa duniani; Yesu aliyetumwa
na Baba yake wa mbinguni ili kuwatangazia maskini habari njema ya wokovu na kwa njia
ya ufukara wake, akawakirimia wote utajiri usiokuwa na kipimo!