Kipindi cha Majilio na Noeli ni wakati wa mshikamano wa dhati na maskini!
Kanisa Katoliki nchini Ubelgiji linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi
mema katika kipindi cha Majilio na hatimaye Sherehe za Noeli, kujitahidi kumwilisha
amri ya mapendo kwa Mungu na jirani, kwa kujitoa kimasomaso kuwasaidia watu wanaolazimika
kuishi katika umaskini, ujinga na maradhi, ili nao pia waweze kuonja huruma na upendo
wa Mungu kwa njia ya jirani zao.
Askofu Jean
Kockerols, wa Jimbo Katoliki la Ypres, Ubelgiji katika barua yake ya kichungaji, anawaalika
waamini pamoja na vyama vya kitume vinavyojitoa kwa ajili ya kuwasaidia maskini, kuendelea
kufanya hivyo kwa ari na moyo mkuu kwani takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya watu
maskini hata nchini Ubelgiji katika kipindi cha Mwaka 2013 imeongezeka kwa asilimia
33.7%. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 5.4% ya maskini nchini Ubelgiji kila mwaka.
Hii ni hali ambayo kamwe haiwezi kukubalika kwani ni kielelezo makini cha ukosefu
wa haki jamii.
Askofu Kockerols anasema, Noeli kiwe ni kipindi cha mshikamano
wa upendo na udugu kati ya watu wa mataifa, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa kupambana na umaskini, ujinga na maradhi. Jamii ijifunze kugawana hata kile kidogo
ilichonacho na wale ambao hawajabahatika kama wao!
Kwa njia hii, Noeli inaweza
kusherehekewa na watu wengi zaidi na wala si kwa wale waliobahatika tu! Kuna idadi
kubwa ya watu wanaoishi katika hali ya umaskini, watu ambao kwao baridi na hali ngumu
ya maisha vimekuwa ni wimbo usiokuwa na kiitikio!