Jimbo kuu la Barcelona limempoteza Kardinali Ricardo Gordò
Kardinali Ricardo Maria Carles Gordò, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Barcelona
na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kuanzia Mwaka 1999 hadi mwaka 2005
amefariki dunia, Jumanne, tarehe 17 Desemba 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Mazishi
yake yanatarajiwa kufanyika Jimbo kuu la Barcelona, Alhamisi, tarehe 19 Desemba, 2013.
Kardinali
Ricardo Maria Carles Gordò alizaliwa tarehe 24 Septemba 1926. Baada ya masomo na majiundo
yake ya Kikasisi, akapewa daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 29 Juni 1951. Baadaye
akaendelea na masomo juu na kujipatia shahada za uzamivu katika Sheria za Kanisa kutoka
katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salamanca, kunako Mwaka 1953.
Tarehe 6 Juni
1969 akateuliwa na Papa Paulo VI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tortosa na hatimaye,
akawekwa wakfu tarehe 3 Agosti 1969. Kama mchungaji mkuu wa Jimbo akajitosa bila ya
kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo lake, kwa kuwashirikisha kwa
namna ya pekee waamini walei ambao walichangia maendeleo na ustawi wa Kanisa, huku
wakiyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.
Tarehe 23 Machi
1990, Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona.
Akiwa anasukumwa na moyo wa kibaba na kichungaji akajenga utamaduni wa mabaraza ya
Mapadre wa Jimbo pamoja na Mabaraza ya kichungaji ili kujipatia utambulisho wa Kikanisa,
kwa kujenga na kuimarisha umoja, ili kwa pamoja waweze kutoka kifua mbele na kuzama
katika mchakato wa Uinjilishaji.
Walengwa wakuu ni Waamini waliokuwa wamesahau
mlango wa Kanisa kwa miaka kadhaa kutokana na sababu mbali mbali; wasioamini ili waweze
kuonja Injli ya Furaha; vijana waweze kutumia karama na nguvu zao kumshuhudia Kristo;
maskini, wahamiaji na familia. Alitafuta, akalea na kukuza miito mitakatifu; akaonesha
kipaumbele cha pekee katika maisha na majiundo ya Mapadre wake tangu wakiwa Seminarini.
Alipenda kuona ushirikiano wa karibu na Maaskofu wake wasaidizi ambao walikuwa
ni wanne, yote aliyafanya kwa sifa na utukufu wa Mungu. Alithamini sana utangazaji
wa Injili kwa njia ya vyombo vya habari. Mwenyeheri Yohane Paulo II alimteuwa kuwa
Kardinali tarehe 26 Novemba 1994.