Ibada zitakazoongozwa na Papa Francisko, Kipindi cha Noeli
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa kesha la Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka
2013. Ibada hii itakayofanyika hapo tarehe 24 Desemba 2013, inatarajiwa kuanza saa
2: 45 za Usiku kwa Saa za Ulaya.
Jumatano tarehe 25 Desemba 2013, Siku kuu
ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, Baba Mtakatifu atatoa
Ujumbe na Baraka za Noeli kwa Mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, kama unavyojulikana
kwa lugha ya Kilatini, "Urbi et Orbi" kuanzia saa 6:00 mchana kwa saa za Ulaya.
Jumanne
tarehe 31 Desemba 2013, Kesha la Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Siku ya
47 Kuombea Amani Duniani, Baba Mtakatifu ataongoza Masifu ya Jioni; Ibada ya Kuabudu
Ekaristi Takatifu pamoja na Kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa kuhitimisha
Mwaka, kama unavyojulikana, "Te Deum".
Jumatano tarehe Mosi, Januari 2014,
Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Maadhimisho
ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani,
ambayo kwa Mwaka 2014 inaongozwa na kauli mbiu "Udugu ni msingi na njia ya amani".
Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 4:00 kwa saa za Ulaya.
Jumatatu
tarehe 6 Januari 2014, Siku kuu ya Tokeo la Bwana au Epifania, Baba Mtakatifu Francisko
kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu.
Taarifa
hii imetolewa na Monsinyo Guido Marini mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini
Vatican, tarehe 17 Desemba 2013.