2013-12-16 09:18:48

Yesu Kristo ndiye kiini na chemchemi ya furaha ya kweli!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kwa Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufurahi kwani Noeli i karibu na kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, hii ndiyo Injili. Kanisa si kimbilio la watu wenye nyuso za kukunjamana bali ni nyumba ya furaha! Kwa wale wenye majonzi wanaonja furaha ya kweli ndani ya Kanisa.

Furaha hii inatokana na utambuzi kwamba, mtu anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu. Huyu ndiye Mungu anayekuja kumkomboa mwanadamu na kuwaganga wale waliovunjika moyo! Ujio wake ni cheche za nguvu zinazomwimarisha na kumkirimia mwamini ujasiri, kiasi cha kuyafanya maua ya kondeni kushangilia, yaani pale ambapo mioyo iliyokauka na kunyauka kama Jangwa inapoonja furaha ya kweli kwa njia ya Neno la Mungu na Roho wake wa upendo.

Waamini wanaalikwa kuwa na ujasiri, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu ili kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa hata kama ni mdhambi kiasi gani! Furaha ya kweli inadumu hata katika majaribu ya maisha kwani inajikita katika sakafu ya moyo wa mwamini anayejiaminisha na kumtumainia Mwenyezi Mungu. Furaha na matumaini ya Kikristo yanajikita katika uaminifu kwa Mungu anayetimiza daima ahadi zake.

Yesu Kristo ndiye kiini na chemchemi ya furaha ya wafuasi wake, changamoto ya kumwendea kwa njia ya Sala na tafakari ya kina, kwa kusaidiwa na maombezi ya Bikira Maria, ili kukutana na Mtoto Yesu, kielelezo cha ukombozi na furaha ya watu wote. Bikira Maria awasaidie waamini kuiishi Injili ya Furaha katika familia na medani mbali mbali za maisha na kwamba, kila mtoto anayezaliwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alibariki Sanamu za Mtoto Yesu zilizokuwa zimebebwa na maelfu ya watoto waliokuwa wamfurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili, tarehe 15 Desemba 2013. Mvua ilikuwa inanyeesha, lakini watoto walionesha furaha ya kukutana na Baba Mtakatifu ili aweze kubariki Sanamu za Mtoto Yesu zitakazowekwa kwenye Mapango ya Noeli.

Amewataka watoto kumkumbuka katika sala zao kama anavyofanya hata Yeye kuwaombea. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa vijana kutoka Zambia, akawataka wawe ni mawe hai kwa ajili ya ujenzi wa Jamii inayojikita katika misingi ya kiutu.







All the contents on this site are copyrighted ©.