Tata Madiba amekamilisha safari ya maisha yake hapa duniani! Apumzike kwa Amani!
Wananchi wa Afrika ya Kusini wanaikumbuka sana Tanzania kutokana na mchango wake katika
harakati za ukombozi kusini mwa Afrika, jambo ambalo limejenga urafiki na undugu wa
dhati kati ya Afrika ya Kusini na Tanzania.
Tanzania chini
ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa mstari wa mbele katika
mapambono dhidi ya ukoloni na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini kwa kuamini
kwamba, binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja.
Padre Dietrich Pendawazima,
Makamu mkuu wa Shirika la Waconsolata, Jumapili tarehe 15 Desemba 2013 amewaongoza
watanzania wanaosoma na kuishi mjini Roma kumkumbuka Tata Madiba aliyezikwa kwa heshima
zote za kitaifa na kimila Kijijini kwake Qunu. Anasema, Mwalimu Nyerere alitamani
sana kuona Bara la Afrika likiwa huru na kwamba, hii ndiyo ingekuwa furaha yake na
chachu ya maendeleo endelevu kwa Bara la Afrika.
Tata Madiba amekamilisha safari
ya maisha yake hapa duniani. Ni kiongozi ambaye ameacha urithi mkubwa kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kusini, Afrika na Dunia kwa ujumla. Watanzania
pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanamhukuru Mungu kwa zawadi ya Tata Madiba
na wanamwombea raha na mwanga wa milele! RIP. Amina.