2013-12-16 10:22:17

Mahojiano maalum kati ya Gazeti la La Stampa na Papa Francisko


Noeli ni kipindi cha matumaini, mapendo na mshikamano. Ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuyaangalia mateso ya mamillioni ya watoto wanaosumbuka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, wakati dunia inaweza kuzalisha chakula cha kuwatosha watu wote.

Kanisa Katoliki katika mikakati yake ya kichungaji linapenda kukuza na kudumisha majadiliano ya Kiekumene na kidini na waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Kanisa linathamini maisha ya ndoa na familia na linapenda kuwasaidia wanandoa kutekeleza wajibu wao barabara kadiri ya mpango wa Mungu, ndiyo maana, Mwezi Oktoba, 2014 kutakuwa na Maadhimisho ya Sinodi Maalum kwa ajili ya Familia.

Haya ni kati ya mambo msingi yaliyojadiliwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahojiano maalum na Gazeti la kila siku la " La Stampa" linalochapishwa kila siku nchini Italia.

Baba Mtakatifu anasema, Noeli ni siku kuu inayomwezesha mwamini kukutana tena na Mwenyezi katika hija ya maisha yake kwa kumkirimia Fumbo la Umwilisho ambalo kimsingi linamwonjesha mwamini faraja na matumaini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kuwaonjesha jirani zao Furaha ya Injili na kamwe wasimezwe na malimwengu na hivyo kujikuta wanatanga tanga kana kwamba ni "daladala iliyokatika usukani"!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Noeli imetekwa na wafanyabiashara wanaotaka kuwaonjesha watu furaha ya mpito ili kuuza bidhaa zao. Furaha ya kweli ya Noeli inabubujika kutoka kwa Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwanadamu anapaswa kutambua kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu.

Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipotembelea Nchi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko anaonesha nia na utashi wa kutaka kutembelea Nchi Takatifu pamoja na kukutana na Ndugu yake Bartolomeo wa kwanza, Patriaki wa Costantinopoli.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna mamillioni ya watoto wanaoteseka bila ya sababu msingi na watoto wenyewe hawatambui kwa nini wanateseka hivi, lakini wanajiachilia katika huruma na upendo wa Mungu. Mateso na mahangaiko ya watoto yanajionesha kwa namna ya pekee kwa watoto wanaoteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, ingawa dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa watu wote.

Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati na watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa pamoja na kubadili mtindo wa maisha, kwa kuwa ni watu wa kiasi badala ya kutupa chakula ambacho kingeweza kusaidia kuganga njaa kwa baadhi ya watu duniani.

Baba Mtakatifu anasema, changamoto anazotoa katika medani mbali mbali za maisha ni utajiri unaobubujika kutoka katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu; mshikamano na maskini; uchumi unaojali mafao ya wengi. Anasema, amewafahamu watu wengi ambao wanafuata siasa za Kikomunisti, ambao ni watu wema na wala hawana hila wala makunyanzi mioyoni mwao. Anasema kwake, haoni shida hata kama baadhi ya watu wanapenda sasa kumwita "Mkomunisti".

Baba Mtakatifu Francisko anabainaisha kwamba, Majadiliano ya Kiekumene na waamini wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo ni kati ya vipaumbele vya pekee kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kuna haja ya kujenga sasa dhana ya "Uekumene wa Damu" kwani damu ni nzito kuliko maji. Kuna maelfu ya Wakristo duniani wanaodhulumiwa na kunyanyaswa bila kujali Madhehebu yao! Umoja wa Kanisa unahitaji neema na baraka kutoka kwa Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuhusu wanandoa walioachana na baadaye kuoa au kuolewa tena ni jambo ambalo Makardinali watalijadili kwa kina na mapana na baadaye Sinodi Maalum ya Familia itaweza kusaidia kubainisha mikakati ya kichungaji inayoweza kuchukuliwa na Mama Kanisa ili kuwasaidia waweze kujisikia kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Serikali na Kanisa ni taasisi mbili zinazopaswa kufanya kazi kwa malengo tofauti, lakini zote zinapania kumhudumia mwanadamu. Anakumbusha kwamba, Siasa ni tendo la upendo; siasa inakuwa ni mchezo mchafu pale inapogeuzwa kuwa ni mahali pa uchu wa mali na madaraka bala ya kuhudumia. Anahitimisha mahojiano maalum na Bwana Andrea Tornielli, mwandishi wa Gazeti la "La Stampa" kwa kusema kwamba, wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kutokana na mchango wao na wala si kugeuzwa kuwa ni Wakleri!

Mahojiano haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.