2013-12-16 08:18:07

Mabalozi wa Vatican ni vyombo vya amani na upatanisho


Kwa mara ya kwanza Askofu mkuu Pietro Parolin, tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 14 Desemba 2013 amemweka wakfu Monsinyo Aldo Giordano kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Venezuela, mahali ambako Askofu mkuu Parolin alitekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican hadi kufikia Mwezi Septemba 2013. Ibada hii imefanyika Jimboni Cuneo, Kaskazini mwa Italia.

Askofu mkuu Parolin ametoa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, anaendelea kulihimiza Kanisa kutangaza Injili ya Furaha. Balozi na wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro wanapaswa kutolea ushuhuda wa ujumbe huu kwa maneno na matendo yao kati ya wakuu wa nchi na Jumuiya za Kikristo wanazozihudumia, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa dhati.

Kama wawakilishi wa Vatican, wanapaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa Kanisa mahalia, kuendelea kuwa ni kiungo makini kati ya Kanisa la Kiulimwengu na Maaskofu mahalia; kwa njia ya utume huu wanajenga na kuimarisha mshikamano na umoja wa Kanisa zima. Ni utume unaohitaji majitoleo na utayari wa kuishi na kukutana na watu kutoka katika tamaduni, hali za maisha kijamii na kikanisa.

Askofu mkuu Giordano kuanzia mwaka 1995 alianza kutekeleza utume wake wa kidiplomasia, kumbe ni kiongozi aliyebobea katika maisha haya na kwamba, changamoto iliyoko mbele yake ni kuendeleza mang’amuzi aliyojipatia katika masuala ya utume Barani Ulaya, ili kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji Mpya Amerika ya Kusini na kwa namna ya pekee kabisa nchini Venezuela.

Askofu mkuu Parolin anasema, huko atakumbana na changamoto za utandawazi, umaskini, ukosefu wa haki jamii, utengano kati ya Kanisa na masuala ya kisiasa; maana ya upendeleo kwa ajili ya watu maskini, umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii na harakati za jamii inayotaka kumng’oa Mwenyezi Mungu katika vipaumbele vya maisha yao. Hizi ni changamoto zilizofafanuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Visiwa vya Carraibi huko Aparecida.

Nchini Venezuela changamoto kubwa ni kuendeleza mchakato waupatanisho, haki na amani; ili kujenga na kudumisha majadiliano na utashi wa watu kukutana pamoja ili kushirikishana tone la matumaini. Askofu mkuu Giordano anaweza kutekeleza vyema utume wake nchini Venezuela kwa kutumia mang’amuzi na uzoefu wa shughuli za kidiplomasia, lakini zaidi aongozwe na mwanga wa Neno la Mungu.

Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na Makardinali 6, Maaskofu 30, wanasiasa na wanadiplomasia kutoka ndani na nje ya Jumuiya ya Ulaya, 30 pamoja na Mameya wa Manispaa kumi na nane.








All the contents on this site are copyrighted ©.