Katika mchakato wa ndoa na familia mhusisheni Mungu na Jamii, msiweke mkataba na shetani!
Tumsifu Yesu Kristo...! Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican; katika kipindi kilichopita
tulianza kuangazia juu ya maandalizi ya kupokea wito wa ndoa na kulijenga Kanisa la
nyumbani. Tulikaza kusema, KWETU SISI TUNAOAMINI, NI MUHIMU KABISA TANGU MWANZO KUMHUSISHA
MUNGU KATIKA MCHAKATO MZIMA NA KATIKA MAISHA YOTE YA NDOA [wapo wanaofanya makosa
ya kumhusisha shetani tangu mwanzo; HAIFAI NI HATARI). Tulihimiza pia wanandoa WAJENGE
UTUME WA KUOMBEANA KWA MUNGU NA KUPELEKANA KWA MUNGU. Hili litarudiwa
tena na tena! Ewe Mwanandoa ni mara ngapi unampigia Mungu goti kumwombea mwenzi wako?
Bahati mbaya wengi huwa tunaombeana yanapotokea matatizo tu. Tukiwa katika heri, sala
zinawekwa likizo. Ewe uliye katika ndoa, kuanzia leo punguza kelele, anza kusali kwa
moyo kabisa kumwomba Mungu kwa ajili ya usitawi wenu na familia yenu. Mlilie Mungu
kwa machozi ya imani; hakika utauona wema wa Mungu. Mungu atakupa nguvu ya kuvumilia,
na kwa uradhi wake, atakuondolea masumbufu hayo. Bwana alisema, ‘majaribu hayana budi
kuja...,’ ndiyo maana twasema WANANDOA WAOMBEANE KWA MUNGU DAIMA, ili yule mwovu anayepanda
mbegu ya chuki na fujo katika ndoa za watu ASIPATE NAFASI KAMWE. Mungu apewe nafasi
ya juu kabisa. Leo tuendelee kwa kuangazia juu ya uhusika wa jamii katika maandalizi
ya kuupokea wito wa ndoa na kulijenga Kanisa la nyumbani. Mpendwa msikilizaji,
kwa vile mwanadamu ni kiumbe jamii, maisha anayoyaishi yana athari pia katika jamii
inayomzunguka. Ndoa ni wito na ni sakramenti ambayo ni muungano halali kati ya [mtu
mume na mtu mke] mume mmoja na mke mmoja, nao wanafanywa kuwa mwili mmoja. Hawa wawili
wanaofanya hesabu ya muungano, hawatoki hewani; wanatoka katika familia au jamaa inayowazunguka.
Katika kuitikia wito wa ndoa, ni vema sana familia ikahusishwa tangu mwanzo. Familia
isishitushwe tu kwamba kuna mtu ameongezeka, au mtu amehama ndani. Jamii isiadhibiwe
kwa kushiriki tu katika matokeo mabaya ya miungano-holela. Kushirikisha jamii ya
karibu kadiri ya taratibu za jamii staarabu; kuna umuhimu wake. Jamii inaweza kuwa
inamfahamu vizuri zaidi huyo unayependa kuwa naye kuliko unavyomfahamu wewe. Jamii
pia inaweza KUKUSAIDIA KUMFAHAMU HUYO MCHUMBA WAKO NA ASILIA YAKE. Ni vema kabisa
umfahamu vizuri huyo unayetaka kuingia naye katika agano ILI USIFANYE MAKOSA YA KUINGIA
KATIKA AGANO NA MTU AMBAYE HUMFAHAMU. Kwa msaada wa jamii yenye nia njema, unaweza
kufanya maamuzi, yenye maana zaidi. Katika hili, tunawaonmba vijana wetu, SHIRIKISHENI
WAZAZI MIPANGO YENU, LISHIRIKISHENI KANISA, MPATE BARAKA YA UCHUMBA. Na wazazi
nao kwa upande wao, waheshimu sana mielekeo sahihi ya watoto wao mintarafu wachumba;
ili WAZAZI NA WALEZI WASIPITILIZE WAKAINGIA KATIKA KOSA LA KUWACHAGULIA WATOTO WAO
WACHUMBA, kwa maslahi yao wazazi wenyewe. Matokeo yake vijana wataingia katika maisha
ya ndoa kwa shinikizo-baridi la wazazi wao. Hapo tangu mwanzo furaha haipo katika
ndoa za aina hiyo. Wazazi na walezi, wasiwakatishe tamaa watoto wao, pale wanapowaletea
habari za maelekeo ya kuupokea wito wa ndoa; lakini pia wasikubali harakaharaka na
kuanza kupiga vigelegele kabla ya kuwasaidia vijana wao kuchunguza mazingira yote
ya wachumba hao. Wazazi watoe miongozo, mafundisho na hata wazee wengine waalikwe
watoe mang’amuzi yao namna ya kuhimili mikikimikiki mbalimbali ya maisha. Hapo kweli
tutakuwa tunawasaidia vijana wetu. Lakini vijana nao wawe tayari kusaidiwa, kukuzwa.
Vijana wasomi wanaweza kukosea, wakadharau mang’amuzi ya wazee ambao hawakusoma.
Kijana mpendwa, mwana wa Kanisa, zingatia neno hili: wazee wetu wana elimu ya mang’amuzi
ambayo haijaandikwa katika vitabu vyovyote ulivyovisoma. UWE TAYARI KUULIZA, KUSIKILIZA,
KUUTAFAKARI USHAURI WA WAZEE NA KISHA KWA BUSARA, KAMA YABIDI HIVYO, KUPOKEA. Tunazidi
kuomba hapa, vijana wetu wawe tayari kuendelea kukuzwa. WASIKUE KABLA YA UMRI. Familia
na jamii ikikwepa jukumu la kuwasaidia na kuwaandaa vijana katika kuitikia wito wa
ndoa na kujenga Kanisa la nyumbani; KAMWE HAITAKWEPA KUONJA MAUMIVU YA MADHARA YANAYOTOKEA
katika miungano isiyo na misingi sahihi. Tunamalizia kipindi hiki kwa kubainisha
kwamba, maisha ya ndoa yenye mwanzo mwema, yatajenga Kanisa la Nyumbani lenye furaha
na matumaini; na kwa lenyewe litakuwa zawadi na fahari kwa jamii inayowazunguka na
tegemeo la Kanisa kwa ujumla. Tunawaweka mikononi mwa Mungu vijana wetu wote. Mungu
awajalie akili tambuzi ya kujua hadhi na uzito wa wito wa ndoa, awajalie utashi imara
wa kuweza kuamua sawasawa na awajalie uradhi wa kuyakubali mapenzi yake katika kuitikia
wito wa ndoa kwa ujasiri; ili MAISHA YA NDOA YASIWE KITU CHA KUDHARAULIWA BALI YAWE
NI TUNU KWA WANADAMU, HESHIMA KWA MUNGU NA TUMAINI LA KANISA. Kutoka katika Studio
za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.