Hati ya kusafiria kutoka kwa Mwalimu J. K. Nyerere kwa Tata Madiba ilikuwa ni chachu
ya mageuzi Barani Afrika!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Baba wa
Demokrasia ya Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela alikuwa pia kiongozi wa Tanzania,
shujaa wa Watanzania na Baba wa wananchi wa Tanzania kama alivyokuwa kwa wananchi
wa Afrika Kusini.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini
zina uhusiano wa kindugu na wa karibu sana kwa sababu ya kazi kubwa iliyofanywa na
waanzilishi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Mzee Mandela.
Rais
Kikwete pia ameelezea historia ya shughuli za ukombozi za Mzee Mandela na jinsi alivyofika
Tanganyika mwanzoni mwa miaka ya 1960, safari ambayo ilifungua msingi mkuu wa mahusiano
kati ya vyama vya siasa za Tanganyika African National Union (TANU) na African National
Union (ANC) cha Afrika Kusini.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza katika mazishi
ya Mzee Mandela yaliyofanyika , Jumapili, Desemba 15, 2013 kijijini kwake Qunu kilichopo
kilomita 23 kutoka mji Mkuu wa Jimbo la Eastern Cape wa Mtata. Rais Kikwete alikuwa
miongoni mwa viongozi wachache walioombwa kuhudhuria hatua hiyo ya Mzee Mandela ambaye
alifariki dunia siku 15 zilizopita nyumbani kwake mjini Johannesburg, akiwa na umri
wa miaka 95.
Katika hotuba yake yenye nguvu na iliyotoa somo la historia, Rais
Kikwete ameelezea jinsi Mzee Mandela alivyowasili mjini Dar Es Salaam Januari mwaka
1962 akitokea mjini Mbeya baada ya kuwa amesafiri bila hati yoyote ya kusafiria kutoka
Afrika Kusini kupitia Bechuanaland (Botswana) na Rhodesia Kaskazini (Zambia).
Rais
Kikwete amesema kuwa safari hiyo ililenga kumshawishi Mwalimu Nyerere kuunga mkono
uamuzi wa ANC kubadilisha mwenendo wa mapambano dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi
kwa kutumia silaha badala ya kuwania haki za Waafrika kwa njia za amani kwa sababu
ilikuwa dhahiri kuwa njia hizo zisingeleta matunda yaliyokusudiwa.
Rais Kikwete
amesema kuwa safari hiyo iliyomwezesha Mandela kupata hati ya kusafiria ya Tanganyika
ambayo ilimpeleka Ghana, Nigeria, Ethiopia na Algeria, ndiyo ilifungua njia ya mabadiliko
ya kidemokrasia yaliyokuja kutokea katika Afrika Kusini mwaka 1994, kuleta uhusiano
wa karibu sana kati ya nchi hizo na kumfanya Mandela kiongozi wa Watanzania kama alivyokuwa
kiongozi wa Afrika Kusini.
Wageni waalikwa walianza kuwasili nyumbani kwa Mzee
Mandela kiasi cha saa 10 usiku na shughuli zenyewe za Mazishi ya Kitaifa ya Rais huyo
wa zamani wa Afrika Kusini zimeanza saa 12 asubuhi ndani ya nyumba ya Mzee Mandela
kwa wanafamilia kuaga mwili wa marehemu kwa mara ya mwisho.
Baada ya kuaga
mwili, wanafamilia wameshiriki ibada fupi na kuandaa jeneza kabla ya kuanza kwa maandamano
ya kupeleka mwili wa marehemu kwenye Hema Maalum kwa ajili ya hatua ya pili ya shughuli
za mazishi, hatua iliyohudhuriwa na wageni maalum waalikwa.
Mwili wa Mzee Mandela
ulifikishwa kwenye Hema Maalum kiasi cha saa mbili na dakika 13 asubuhi, siku ya Jumapili
tarehe 15 Desemba 2013 kwa ajili ya Sherehe ya Kwanza ya Mazishi ya Kitaifa katika
historia ya Afrika Kusini na kuwekwa chini ya jukwaa kuu ambalo lilipambwa na mishumaa
95 iliashiria umri wa Mzee Mandela wakati anaaga dunia wiki mbili zilizopita Desemba
15 nyumbani kwake mjini Johannesburg.
Mazishi ya leo ambayo yameendeshwa kwa
mchanganyiko wa mila na desturi za Kabila la Xhosa na Kanisa la Methodist ambalo Mzee
Mandela alikuwa mwamini wake yamekamilisha siku 10 za maombolezo ya kiongozi huyo,
maarufu kwa jina la Baba wa Demokrasia ya Afrika Kusini.
Miongoni mwa watu
ambao wamezungumza kwenye shughuli hiyo na kuvutia sana watu alikuwa ni Mzee Kenneth
Kaunda, Rais wa zamani wa Zambia na Mzee Ahmad Kathrada, mwanasiasa ambaye alifungwa
kwenye jela ya Robben pamoja na Mzee Mandela.
Mzee Kathrada ambaye anasema
kuwa alikutana na Mzee Mandela miaka 67 iliyopita, alifungwa Robben kwa miaka 26 wakati
Mzee Mandela alikaa miaka 27. “Alipofariki Walter Sisulu nilikuwa nimepoteza baba
yangu, sasa kwa kumpoteza Nelson Mandela nimempoteza kaka yangu. Sina mwingine aliyebakia
wa kumkimbilia,” alisema Mzee Kathrada katika kauli iliyovutia sana hisia za waombolezaji.
Miongoni
mwa wageni hao maalum waalikwa walikuwa ni pamoja na Rais Kikwete na viongozi kutoka
nchi mbalimbali chache wakiwemo wa Malawi, Zambia, Nigeria, Zimbabwe, Lesotho, Ethiopia
na Mama Maria Nyerere. Kwenye hatua hii ya pili, wageni maalum wamesikiliza nyimbo
za kwaya na hotuba mbalimbali za viongozi wachache waliopewa heshima maalum ya kuzungumza
katika shughuli hiyo akiwemo Rais Kikwete.
Wengine waliozungumza ni mwakilishi
wa familia ya Mandela Chifu Ngangomhlaba Matanzima, rafiki wa karibu wa Mzee Mandela
Bwana Ahmad Kathrada, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa
Hailemariam Daselegn, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC)
Rais Joyce Banda wa Malawi na Rais mwenyeji Mheshimiwa Jacob Zuma.
Baada ya
hatua hiyo ya pili, mwili wa Mzee Mandela umehamishiwa kwenye kaburi lake ukiwa unashuhudiwa
na waombolezaji maalum ambao ni pamoja na familia yake. Kwenye eneo hilo la kaburi,
Ofisa wa Jeshi la Afrika Kusini ameondoa medali, bendera na heshima nyingine ambazo
kiongozi huyo amewahi kuzipata katika maisha yake na kuzikabidhi kwa Mkuu wa Jeshi
hilo ambaye naye amezikabidhi kwa Rais Zuma ambaye amezikabidhi kwa mrithi wa Mzee
Mandela.