Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, tarehe 12 Desemba 2013 amewaongoza wananchi wa Kenya
kusherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu walipojipatia uhuru wa bendera kutoka kwa Mwingereza.
Wananchi wamepongeza maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana nchini Kenya na kusema
kwamba, Kenya ingeweza kuwa imefika mbali kama rushwa, ufisadi, utawala mbaya na ukabila
vingekuwa vimevaliwa njuga tangu awali!
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa
sasa inajielekeza katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; maadui watatu
waliotambuliwa tangu Kenya ilipojipatia uhuru wake wa bendera miaka hamsini iliyopita
chini ya Hayati Rais Jomo Kenyatta. Sherehe hizi zimehudhuriwa na wakuu wa nchi 14.
Mizinga 21 ilipigwa kama kielelezo cha shamrashamra hizi pamoja na gwaride
la vikosi vya ulinzi na usalama kutoka Kenya vilivyoonesha ukakamavu mkubwa. Kenya
inaendelea kucharuka katika uchumi, biashara na miundo mbinu. Jubilee ya miaka 50
ya Uhuru wa Kenya iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu: mafanikio, matatizo
na changamoto zilizoko ili wananchi wa Kenya waweze kucharuka katika maendeleo yanayotoa
kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, binadamu na utu wake.
Rais Uhuru
Kenyatta katika hotuba yake wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru
wa Kenya amesema, Serikali yake itaendelea kukazia ukweli na uwazi; inawahimiza wananchi
kuchapa kazi kwa bidii, juhudi na maarifa na kamba, itawashughulikia bila huruma mafisadi
na wote waliojipatia utajiri kwa njia isiyo halali na kwamba, kwa sasa kipaumbele
cha kwanza ni utawala bora!