2013-12-12 11:40:04

Yaliyojiri Bonde la Ufa katika kufunga Mwaka wa Imani!


Parokia za Chibumagwa na Kintinku zote za Jimbo Katoliki Singida-Tanzania, zimefunga rasmi mwaka wa imani sanjari na mwaka wa Makatekista. Misa takatifu ilifanyika katika parokia ya Kintinku. Mbali na mambo mengine katika ibada hiyo ilitolewa tathmini jinsi walivyoishi mwaka wa imani.

Aidha, Makatekista 45 walitunukiwa vyeti vya utambuzi wa utume wao uliotukuka katika kanisa. Ili kukamilisha vizuri mwaka wa imani, Wakatekumeni 4 walipiga hatua yao ya kwanza katika maandalizi yao ya ubatizo hapo mwaka kesho katika vijilia ya Pasaka. Lakini pia katika ibada hiyo ndoa moja ilifungwa ili kudhihilisha uimara na kukua katika imani kwa kupiga vita ndoa za gizani na mitala.

Waamini wengi toka katika Parokia hizo mbili walikuwepo. Maandamano yalianza saa 1:45 asubuhi na misa ilianza saa 3:00. Kwaya mbalimbali zilifika kuboresha ibada takatifu. Katika parokia ya Chibumagwa zilitoka kwaya tatu na Kintinku kwaya tatu. Kulikuwepo vyama mbalimbali vya kitume kama vile Utoto Mtakatifu, WAWATA, UMAKASI, VIWAWA, nk. Yote haya yaliipamba siku hiyo na kuifanikisha.
UTANGULIZI
Utangulizi wa ibada ya misa takatifu ulitolewa na Pd. Henry Nilla, C.PP.S. Akiwaalika waamini katika adhimisho la misa alisema: katika adhimisho la Misa Takatifu siku ya leo tuna mambo makuu mawili; kwanza kabisa tunaungana na Kanisa zima kuadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Andrea Mtume, aliyeitwa na Kristo akaacha kazi yake ya kuvua samaki akamfuata na akatumwa kwenda kutangaza habari njema.

Pili katika Parokia zetu za Chibumagwa na Kintinku tunafanya maadhimisho ya kufunga mwaka wa imani. Katika kuuishi mwaka wa imani, mama Kanisa amekuwa akiwasisitiza watoto wake juu ya mambo msingi na ya muhimu kuhusu imani kama vile, sala, kupokea sakarmenti za kanisa, kusoma neno la Mungu kulitafakari na kuliishi, katekesi, matendo ya huruma na hija. Mambo hayo tukiyazingatia na tukayaishi yatatusadia kuishi vema imani yetu.

Tunapofunga Mwaka wa Imani haimaanishi kwamba sasa ni mwisho wa kuiishi imani yetu bali ndiyo mwanzo mpya wa kuyaweka katika matendo yale yote tuliyofundishwa na mama Kanisa katika mwaka huu. Katika adhimisho la misa ya leo tunapenda kutambua kazi nzuri na njema ya kufundisha imani inayofanywa na makatekista wetu, tunawapongeza sana na kanisa linathamini sana mchango wao katika kufundisha imani katoliki. Kama ishara ya kuonesha shukrani zetu tutawapatia vyeti maalum ambavyo vitakuwa ni kumbukumbu kwao katika utumishi wao uliotukuka katika Kanisa.

Tumwombe Mungu atujalie neema zake ili sisi sote tuweze kuiishi kiaminifu imani yetu.

SEHEMU YA MAHUBIRI KATIKA IBADA YA KUFUNGA MWAKA WA IMANI
Katika mahubiri yake Pd. Moses Gwau, Paroko wa Parokia ya Kintinku, alisisitiza juu ya kufunga mwaka wa imani bila kufunga imani. Mwaka wa imani unapofungwa haina maana kwamba tumemaliza kupokea, kuishi, kujifunza zaidi, kushuhudia, kutetea na kushirikisha imani yetu katika ukweli. Tulichomaliza ni kipindi ambacho kiliwekwa kwa ajili ya kujikumbusha misingi yetu ya imani kwa nguvu zaidi. Kwa hiyo mwaka huo uliowekwa ndio umemalizika lakini imani inaendelea.

Mwaka huu wa imani tunaohitimisha ulianza mwaka 2012 pale Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI, alipoutangaza rasmi kuwa ni mwaka wa Imani kwa hati yake "PORTA FIDEI" maana yake "Mlango wa Imani." Kanisa katika mwaka huo mzima lilifanya pia kumbukumbu ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican na pia miaka 20 tangu kuchapishwa rasmi Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Hayo ndiyo baadhi ya mambo muhimu yaliyotuongoza katika Mwaka wa Imani.

Mwaka wa Imani ulitualika kuvumbua upya na kujifunza misingi ya imani. Ulikuwa ni mwaliko wa uongofu wa kweli wa ndani. Katika kipindi hicho chote tulilenga kuamsha ndani ya moyo wa kila mwamini, hamu ya kukiri imani kikamilifu kwa kujiamini, na kwa matumaini. Kazi ambayo tunaamini tumeifanya vizuri.

Lakini pia katika mwaka huu wa imani tulialikwa kutafakari kwa makini juu ya safari yetu pamoja na Mungu, na kujipima ni kwa kiasi gani tumekua na kukomaa katika imani. Ulikuwa ni mwaka wa kufanya tathmini ili kuona ni kwa namna gani tumekua na kubadilika katika imani au bado tuko watoto mbali na kipindi chote hicho cha safari ndefu tangu tumepokea imani.

Kipindi hiki kilikuwa pia, cha kuhuisha imani zetu katika liturjia na hasa katika Ekaristi takatifu, Sakramenti ya Kitubio, pamoja na Sakramenti nyingine zote. Tofauti na wakati mwingine, mwaka huu wa imani, tuliendelea kulisoma Neno la Mungu na kushibishwa nalo. Ndiyo maana ulikuwa ni wakati maalum. Leo tunapofunga mwaka imani, ni mwanzo wa safari ya kudumu ya imani kwa waamini wote katika Kanisa.

Imani inatusadiaje? Imani inatusaidia kupata wongofu wa ndani, na wa kweli. Imani ya kweli bila wongofu haitoshi. Kwa hiyo mtu akisema kuwa ana imani kwa sababu tu anafanya maadhimisho mbali mbali, bila kuwa na wongofu wa kweli imani hiyo haisaidii kitu chochote. Hivyo imani inatusaidia kupata wongofu wa ndani, na wongofu wa ndani unaendana na maisha ya kila siku ya kila mwamini. Imani ni lazima itupatie wongofu. Kama haitupatii wongofu inabaki ni makelele tu.

Kufikiri kuwa kwa imani peke yake tunafanyika warithi wa Kristo bila kuteseka na kutakatifuzwa naye hakutoshi. Hatuwezi kuwa warithi wa mbingu bila kuwa waongofu. Hawa hujidhihirisha katika maisha yao, kazi zao, hapo ndipo imani na wongofu humfanya mtu mrithi pamoja na Kristo.

Kristo anatualika mara kwa mara akisema kuwa anayetaka kuwa mfuasi wake lazima achukue msalaba amfuate. Kumbe ni lazima kuteseka na Kristo. Lazima kutakatifuzwa naye. Haya yatawezekana katika imani, ambayo imetuongoza kwa mwaka mzima.

Mfano wa wanariadha ambao Mtume Paulo anautumia vizuri katika maandiko matakatifu, unaonesha wazi kuwa wanariadha wote wana lengo la kushindana ili wapate tuzo. Hawafiki uwanjani kufanya utani au bila kuwa na nia ya kushinda. Wako wengi wanariadha, ndiyo maana hakuna mashindano ya mtu mmoja tu. Nia na lengo la washindanao ni kupata ushindi. Ndiyo maana inapotokea kuwa wameshindwa wengine hujiua, hulia, hupoteza matumaini, hulaumu wengine, nk. Kumbe ukweli ni kwamba kati ya hao wanaoshindana kuna wanaoshinda. Mtu mmoja kati yao anashinda, kwa huruma unaweza kusikia wameongezea na wa pili au wa tatu.

Wanariadha hukimbia kwa malengo, na sio kwenda tu! Wala sio kukimbilia mahali popote bila utaratibu au sheria zinazowaongoza. Wanakuwa na utaratibu fulani ili wasiingilie mistari ya watu wengine eti kwa sababu wanafanya mashindano. Wanariadha wanafanikisha malengo kwa kufanya maandalizi na mazoezi mengi; ndiyo maana mtu mmoja aliwahi kusema kuwa kama angepewa masaa 6 ya kukata mti mkubwa, angetumia masaa 4 kunoa shoka na mapanga.

Sisi tunashinda katika imani kwa kubaki waaminifu kwa njia ya kukiri wito wetu na uteule wetu kwa njia ya kazi zetu njema, ndiyo mazoezi yenyewe. Kazi njema itokanayo na kuamini ndiyo itatupatia kibali cha kushinda baada ya maisha haya. Kumsifu na kumtukuza Mungu ni malengo ndani ya mpango mzima wa kuishi imani. Tunapofikiri kupata zawadi ya uzima wa milele kama wana riadha wanaofikiri kupata zawadi ya ngao au tuzo fulani sisi nasi kwa kupitia kazi zetu njema tunafikiri kupata zawadi ya uzima wa milele pale tunapojikita katika malengo yetu msingi ya kumsifu na kumtukuza Mungu katika maisha yetu.

Bila imani hatuwezi kumridhia Mungu. Na imani peke yake haitoshi. Hatuwezi kumpendeza Mungu bila imani. Mtu mwenye imani husadiki kuwa Mungu yupo na huwatuza wale wanaomtafuta kwa moyo mnyoofu. Hata kama ungekuwa unafanya kazi njema, unalitegemeza kanisa, unatoa michango, unawajali maskini, nk. Bila imani hamna kitu bali hayo unayoyafanya ni mazuri ila yanabaki ni kama shughuli za kijamii tu. Ndiyo maana imani na matendo vinadai kwenda pamoja. Imani na kazi njema ni pande mbili za shilingi, (Heb. 11:6). Tunaalikwa kudumu katika imani.

Siku hizi kumezuka makundi mengi, vikanisa vingi vimeanzishwa, makundi ya kiibada, nk. Hivi vimewafanya baadhi ya waamini wenye imani haba kuanza kutangatanga. Leo wapo hapa kesho pale, na hasa wanaposikia kuwa kuna sehemu nyingine wanagawa mahindi, uwele, pesa, mikopo, magari, nk. Imani sio kitu cha kuonja hapa na kuonja pale. Imani inatudai udumivu hadi mwisho (Mt. 10:22). Atakaye dumu hadi mwisho ndiye atakayeokoka. Maisha ya kuonja onja hapa na pale Kristo anatoa majibu.

Tutafute wokovu kwa hofu na tetemeko. Hatutafuti wokovu kwa muda na mahali tunapotaka, bali tunaalikwa kujishughulisha na wokovu wetu ambao una thamani kubwa. Hivyo hatuwezi kuuthamanisha na kilo moja ya mtama au mahindi. Wokovu unapatikana kwa njia ya sala, kazi, majitoleo, kufunga, na usafi wa moyo. Haya yote yanatupatia tumaini kwa Mungu, na si tumaini katika mtama.

Mwaka huu tumetafakari mambo mbalimbali. Ndani ya hizo tafakari tumeona kuwa ukristo wetu ulivyo na changamoto nyingi leo. Changamoto iliyokubwa ni vivutio vya kidunia. Kwa mfano tunatambiana kwamba kanisani kwenu hawatendi miujiza, hawatoi pepo, hawaponyi watu, hawagawi fedha, hawaombei watu ili kupata magari. Vivutio vimekuwa changamoto kubwa sana!

Bila uchumi mzuri mkristo anajiona hawezi kuwa mkristo mzuri kwa sababu kwake yeye cha msingi ni apate uchumi mzuri kwa kuwa na imani. Kwa kuwa na imani asiugue, asifirisike eti kwa sababu ana imani, asife, asikose kazi, nk. Vivutio hivi pamoja na makundi mbalimbali yamekuwa maarufu nyakati zetu. Je, unataka hela? Ingia kikundi fulani. Unataka uchumi mzuri, fedha, nyumba, gari, ingia kundi fulani upate hayo yote na zaidi.

Vivutio hivi, vyaweza kutupotosha au kufifisha kazi ya wokovu inayopatikana kwa njia ya msalaba. Vivutio vyenyewe vinaeleza kwamba maisha ni hapa hapa duniani, hakuna maisha mengine baada ya haya. Ponda mali kufa kwaja! Maelezo hayo yanaweza kupamba vizuri maisha haya kiasi kwamba mtu wa imani haba akapotoka. Vivutio hivi ni rahisi kutusahaulisha kwamba Kristo hakutukomboa kwa dhahabu na fedha bali kwa mateso kifo na ufufuko. Kifo juu ya msalaba. Kazi yetu kubwa ni kupambana na kupigana vita pamoja na Kristo. Kumpinga shetani na hila zake mbaya.

Katika enjili tumesikia juu ya kuitwa kwa mitume. Yesu aliwaita mitume ili akae nao, awafundishe na hatimaye awatume; leo tumesikia wito wa Mtume Andrea. Andrea alikuwa mwanafunzi wa Yohane mbatizaji na ndiye aliyewatambulisha kwa Yesu. Akasema "tazama mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia", ndipo wakaenda kwa Yesu. Na Yesu akawauliza mnatafuta nini? Wakamuuliza Bwana unakaa wapi? "Akasema njooni nanyi mtaona." Wakaenda, wakashinda naye siku ile. Walishinda naye sio walikwenda kuona tu. Unaweza kuwa na imani, ukaona lakini usishinde na Yesu.

Pia Yesu aliwaita wana wa Zebedayo na kuwaambia, njooni mnifuate nami nitawafanya wavuvi wa watu. Mitume hao waliacha nyavu zao, wakamfuata. Hawa walimwacha baba yao pia. Waliacha vivutio vya kuwasaidia ili wafurahie maisha, wakaacha nyavu zao. Wamfuate kwa sababu gani? Hawa walikuwa na ajira tayari ya kuwapatia mahitaji. Tena inasemekana kuwa walikuwa na uwezo wa kupeleka samaki wao kwenye masoko makubwa na kupata fedha nyingi. Lakini wanaacha na kumfuata huyu asiyeeleweka, hana biashara, hana uchumi uliokomaa hadi hana hata mahali pa kulaza kichwa chake.

Katika mwaka huu tumetafakari juu ya ubatizo wetu pale ambapo Bwana alipotuita kwa njia ya imani tumfuate,tumeona anapokaa, sasa mwaliko mkubwa ni kushinda naye. Je, tumeshinda naye katika nini? Katika sala, majitoleo, mafungo, usafi wa moyo na mengine mengiā€¦Hii inatufanya tuathiri vivutio vingine ambavyo vingetufanya tuhadaike kuwa kwa Kristo hakuna msalaba. Ulimwengu unatafsiriwa kuwa ni mahali ambapo hakuna mateso, ni furaha, hakuna msalaba, hakuna huzuni, lakini tusisahau kuwa Yesu ambaye ndiye mwalimu wetu anasema kuwa anayetaka kumfuata ni sharti ajitwike msalaba wake amfuate.

Katika ulimwengu wa leo kuna mitego mingi ukilinganisha na nyavu zile walizotumia mitume. Kumbe kupokea wito ni kujiambatanisha na Kristo mwenyewe, kujibandika kwa Kristo kana kwamba una gundi. Kujinatisha kwa Kristo. Mwito wa Kristo sio kujiambatanisha bali kujibandika kwake kama mitume walivyoona wakaambatana naye.

Pd. Mulokozi Deusdedit, C.PP.S., Paroko wa parokia ya Bikira Maria Mpalizwa-Chibumagwa kabla ya kugawa vyeti kwa Makatekista aliwakumbusha waamini mambo msingi katika mwaka wa imani na kusema: tusisahau kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ilikuwa ni uinjilishaji mpya kwa ajili ya kueneza imani ya ukristo. Tusimame imara katika imani yetu. Nembo ya mwaka wa imani ilikuwa ni mtumbwi/mashua ambayo haiko nchi kavu bali iko majini tayari imekwishaanza kusafiri na abiria wake ni sisi sote yaani kanisa linalosafiri.

Petro na wenzake walipokuwa wanavua samaki usiku kucha wasipate kitu na Yesu anawaambia kuwa watweke kilindini, Petro alishangaa kama mtaalam wa uvuvi. Aliona kwamba haiwezekani kupata samaki mchana. Alijua kuwa samaki wanapatikana usiku. Lakini alitamka "kwa imani nitafanya." Tweka hadi kilindini ndivyo tunavyoaswa sote na mama kanisa leohii. Makatekista wanarudia kusikia neno hili la tweka hadi kilindini pale mlipo, anza safari, ndani ya kanisa linalosafiri ili kuongoza watu wa Mungu mliopewa. Huo ndio wajibu wetu. Tuwasaidie makatekista wetu ili tuweze kusafiri pamoja, tuweze kulinda imani yetu pamoja.

Katika kanisa hili linalosafiri bado tuna nembo nyingine moja, mlingoti wake ni msalaba, na penye msalaba pameandikwa Yesu mwokozi wa wanadamu. Yeye ndiye kiongozi wetu. Wengine walitetereka baada ya kuona mawimbi, wakalalama kuwa wanaanza kuzama. Msiogope, timiza wajibu wenu, shika imani yenu, ili tuweze kuhubiri vizuri tunahitaji kuwa na elimu sahihi juu ya imani yetu, elimu ambayo hakuna mtu anayeitilia mashaka.

Tukiwa kwenye mtumbwi tusichoke kuinua macho yetu kwenye mlingoti ambaye ni Kristo mwenyewe, mwokozi wa wanadamu. Tufundishe imani sahihi, imani katika Kristo Yesu. Tusihofu hata kama tutakuwa na kigugumizi kwani kaa la moto wa Mungu yaani elimu sahihi itatufanya, tuishi, tusimame imara kuihubiri na kuifundisha kwa uhakika.
Makala hii imeandaliwa na
Pd. Mulokozi Deusdedit, C.PP.S.
Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa-Chibumagwa
Jimbo Katoliki Singida-Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.