Papa- utu wa binadamu ni lazima kutetewa na kulindwa...
Baba Mtakatifu Alhamis hii majira ya asubuhi, aliwakaribisha na kuwahutubia, mabalozi
waliowasilisha barua zao za utambulisho , kwa Jimbo Papa, tokea nchi zao. Mabalozi
hao ni kutoka Algeria , Iceland, Denmark, Lesotho, Palestina, Sierra Leone , Cape
Green , Burundi , Malta , Sweden , Pakistan, Zambia , Norway, Kuwait, Burkina Faso,
Uganda na Yordan.
Katika hotuba yake, Papa aliwashukuru kwa salaam za matashi
mema toka kwa viongozi wa nchi zao , na hivyo nae pia aliutumia muda huo kupeleka
salaam zake kwa wakuu wa nchi hizo na pia kwa raia wote wa nchi zao.
Papa
katika hotuba yake, alilenga zaidi matatizo na maovu yanayofanyika katika jamii ya
nyakati hizi zetu, na hasa tatizo la watu kurubuniwa na kusafirishwa nje ya nchi
zao kwa ahadi za uongo ambako heshima ya utu wao hudharirishwa na kutumikishwa nje
ya ubinadamu. Na ametoa wito kwa jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu zake , kwa
ajili ya kupambana na matatizo hayo.Papa ameonyesha imani yake kwamba, kwa juhudi
za pamoja, madhulumu mengi dhidi ya haki za binadamu yanaweza kukomeshwa . Kupitia
Mabalozi hao,ameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi zake katika kutetea usawa,
na kuwa na mkakati madhubuti wa kukomesha usafirishaji haramu wa watu, unaosikika
kila sehemu ya dunia, hata katika nchi zenye viwanda vingi. Amekemea wanaume na wanawake,
kutumiwa, kama chambo cha uchumi.
Adiha Papa pia ameonyesha kujali na kuitaka
jumuiya ya kimataifa kuweka kipaumbele cha kwanza, katika mipango ya kufanikisha
amani , mazungumzano na mahusiani mazuri kitamaduni, kisiasa , kiuchumi, na kujaribu
kuyakoa maisha ya watu yanayo hatarishwa na matatizo mbalimbali.
Papa alieleza
na kuonyesha kati ya masuala yanayomtia wasiwasi zaidi na ni ugandamizaji wa utu
wa binadamu, kunakoonekana katika mfumo mpya wa usafirishwaji haramu wa watu, ambao
ni aina mpya ya utumwa mambo leo , tatizo linalozidi kupanua makucha yake, ambalo
lipo katika mataifa yote hata yaliyo endelea, na hugusa zaidi watu walio katika mazingira
magumu kijamii: wanawake na wasichana , wavulana na wasichana , walemavu, maskini,
ambao wengi wao ni kutoka familia maskini na wale wanao dharirishwa na migawanyiko
ya kijamii .
Papa alisema, kwa Wakristo, huiona sura ya Yesu Kristo mteswa
kwa watu hao wanaoteseka, wengi wao wakiteswa na umaskini na udhaifu wa kihali, akisema
hata nje ya mtazamo wa imani ya kidini, kwa jina la ubinadamu wa kawaida, huonekana
haja ya kushiriki kwa huruma, mateso ya watu hao wanyonge, kupitia utendaji wa hiari,
wenye kujali mahangaiko yao.
Papa amesema kwa pamoja, ni lazima sote kuwa
na jitihada za kuleta ukombozi dhidi ya mateso haya na hasa katika kukomesha biashara
ya kutisha ya watu kusafirishwa na walaghai wachache wenye uchu wa fedha, wenye kuwaigiza
mamilioni ya wahanga katika kazi ya kulazimishwa au kwa lengo la unyonyaji wa kinjisia
na ngono.
Papa amekemea haya hayawezi kuendelea kuachwa hivihivi kama ilivyo,
maana ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Ni ukiukwaji wa utu wa mtu ,na ni kushindwa
kwa jumuiya ya kimataifa.
Papa ameonyesha imani yake kwamba, jumuiya ya kimataifa,
inao uwezo wa kukomesha hayo , iwapo itasimamia vyema uwepo wa usawa na mkakati madhubuti
dhidi ya usafirishaji wa watu.
Na aliwaahidi Mabalozi kwamba, Jimbo la Papa
liko tayari kutoa kila msaada unaoweza kuhitajika toka idara mbalimbali za Curia
ya Roma, katika utendaji wa kazi zao. Na aliwatakia wingi wa baraka za Mwenyezi
Mungu .