Hali bado ni tete Kaskazini mwa Mali na matumaini ya hali ya amani kurejea tena katika
siku za hivi karibuni yanaonekana kufifia baada ya mapigano makali kuzuka kati ya
Jeshi la waasi na vikosi vya wanajeshi kutoka Ufaransa, vilivyoko nchini Mali ili
kulinda amani na utulivu.
Mapigano haya yamepekea watu kadhaa kupoteza maisha
yao na taarifa za kijeshi kutoka Ufaransa zinaonesha kwamba, Vikosi vya waasi vina
uhusiano wa karibu na Kikundi cha Kigaidi, kilichojitwalia madaraka Kaskazini mwa
Mali kunako mwaka 2012. Vikosi vya kijeshi kutoka Ufaransa vitaendelea kuwepo nchini
Mali hadi hali ya amani na utulivu itakaporejea tena.
Juhudi za kulinda amani
zinasimamiwa pia na vikosi vya kulinda amani kutoka Umoja wa Afrika. Bado kuna kinzani
na migogoro ya kijamii nchini Mali, baada ya mapinduzi ya Serikali yaliyofanyika kunako
mwaka 2012.