Maelfu ya wanafamilia, viongozi wa serikali, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, watu
mashuhuri, wageni na wananchi wa Afrika ya Kusini wanaendelea kutoa heshima zao za
mwisho kwa mwili wa Marehemu Mzee Nelson Mandela aliyefariki dunia hapo tarehe 5 Desemba
2013 akiwa na umri wa miaka 95. Mwili wake umelazwa kwenye Jengo la Serikali, mjini
Pretoria, mahali ambapo miaka 19 iliyopita aliapishwa kuwa Rais wa kwanza Mzalendo
nchini Afrika ya Kusini. Miaka 27 gerezani chini ya utawala wa Ubaguzi wa Rangi
Afrika ya Kusini. Kunako Mwaka 1990 akawaomba wananchi wa Afrika ya Kusini kujikita
katika haki, msamaha na upatanisho wa kitaifa. Mwaka 1994 akachaguliwa kuwaongoza
wananchi wa Afrika ya Kusini, katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo,
utawala wa ubaguzi wa rangi ukatoweka! Kwa siku ya Jumapili, macho ya wengi yataelekezwa
Mashariki mwa Jimbo la Cape. Ndege ya kijeshi nchini humo itachukua mwili wa Mandela
kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Pretoria hadi Mthatha, katika Jimbo la Mashariki ya
Cape. Maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kujipanga kwenye mitaa kuanzia uwanja wa
ndege wa mji huo, maarufu Mthatha kwa ajili ya kuangalia wanajeshi wanavyosafirisha
mwili wa Mandela ukiwa kwenye jeneza kwenye gari la mizinga kuelekea kwenye kijiji
cha Qunu, kilichopo Jimbo la Cape Mashariki ambako kiongozi huyo alilelewa tangu akiwa
mtoto