2013-12-11 14:01:08

Vita dhidi biashara haramu ya dawa za kulevya!


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo mbioni kutunga sheria ya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kuwashawishi wauzaji wadogo kuwataja waagizaji wakubwa wa dawa hizo. Pamoja na sheria hiyo pia wanatarajia kuweka kitengo maalumu kitakachoshughulikia kesi za dawa za kulevya ili kuharakisha hukumu za kesi hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge William Lukuvi alisema hayo mapema juma hili alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari kuhusu taarifa ya hali ya dawa za kulevya vya mwaka 2012.

Waziri Lukuvi alisema bado biashara hiyo imekuwepo hapa nchini licha ya juhudi mbalimbali dhidi ya wafanyabiashara hiyo haramu. Alisema kutokana na kuongezeka kwa biashara hiyo serikali inaangalia uwezekano wa kutunga sheria kali zaidi ikiwemo kumuomba Jaji Mkuu kutenga kitengo maalumu cha kushughulikia kesi hizo.

Alisema katika nchi mbalimbali kumekuwa na sehemu maalumu ya kushughulikia wanokamatwa na dawa hizo huku akitolea mfano nchi ya Bangladeshi ambayo wamekuwa na mahakama na mahakimu katika viwanja vyake vya ndege wanaoshughulikia dawa hizo. ‘’Sisi hapa nchini tumegundua bado kuna mianya ya kuwafanya watu wanaokamatwa kupata mianya ya kutorokea hivyo tunaangalia kuweka sheria kali zaidi manake hata kama ukimkamata mtu hapa kwetu ni lazima mkemia mkuu athibitishe’’ alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema mpaka sasa imeonyesha kuwa biashara hiyo haifanyiki kwa kiasi kikubwa hapa nchini bali Tanzania imekuwa ni njia ya kupitisha dawa hizo kwenda nchi zingine. Akizungumzia ukamataji wa dawa za kulevya Lukuvi alisema kiasi cha hekari 214 za mashamba ya bangi ziliteketezwa katika kipindi cha mwaka 2012 ukilinganisha na hekari 23 mwaka 2011.

Alisema katika kipindi cha mwaka jana jumla ya kilo 211 za dawa aina ya Heroin zilikamatwa huko Mkoani Lindi ikiwa ni kiasi kikubwa kuliko chote kilichowahi kukamtwa kwa mkupuo hapa nchini. Waziri huyo alisema serikali pia iliendelea na jitihada za kuziharibu dawa za kulevya zilizokamatwa nchini kwani kiasi cha kilo 96.8 za heroin na Cocaine ziliteketezwa baada ya kesi husika kutolewa hukumu. Kesi hizo zilitolewa hukumu katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na Lindi na uteketezaji huo ulifanywa kwa ushirikiano wa vyombo vya dola.








All the contents on this site are copyrighted ©.