2013-12-11 15:08:02

Papa asema hukumu ya mwisho ni mwanzo wa faraja na furaha kuu...


Baba Mtakatifu Francisko katika mfululizo wa mafundisho yake juu ya sala ya Nasadiki , leo amezungumzia maneno ya mwisho , “nasadiki katika uzima wa milele. Amesema ni maneno ya mwisho yanayorejea ujio wa pili wa Bwana, katika utukufu, kwa ajili ya kuhukumu wazima na wafu , ambamo sote tutawajibika mbele ya Mungu kwa mazuri au mabaya tuliyoyafanya katika maisha yetu.

Papa alieleza na kurejea neno la Mungu, kama ilivyoandikwa katika Injili ya Mathayo : "Kisha Kristo atakuja katika utukufu wake pamoja na malaika wake wote ... Na mbele yake, watakusanyika mataifa yote na Yeye atawatenganisha mmoja na mwingine kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi , akiweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wa kushoto ... Na kisha atawaambia walio mkono wa kulia njoni ninyi mliobarikiwa na Baba Yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari..Na atawageukia walio mkono wa kushoto akisema, ondokeni kwangu ninyi mlio laaniwa ,mwende katika moto wa milele. Mliowekewe tayari na Ibilisi na malaika zake..... (Mt 25,31-33.46 )".

Papa amefafanua kuwa, mara nyingi , tunaposikia au kufikiri juu ya kurudi kwa Kristo na hukumu yake ya mwisho, ambamo kila mmoja atawasilisha matunda ya kazi yake katika hukumu hii ya mwisho wa maisha , tunaingiwa na wasiwasi, mashaka na hofu. Hakuna sababu ya kuogopa. Ni kuwa na imani, kama Kanisa linatualika kuliona hilo kwa mtazamo chanya, kwamba hukumu ya mwisho ni mwanzo wa faraja na tumaini kuu la furaha.

Papa alieleza na kutoa mwaliko mwaliko kwa Waaamini wote, akitazamisha katika Wakristu wa mwanzo , ambao walilisherehekea tumaini hili kwa kutumia maneno “maranatha”,wakiita hima ujio wa pili wa Yesu, kama mwanzo wa sherehe kubwa ya Arusi ya ubinadamu katika kujipatanisha na Mungu. Na kwamba, katika Siku ya Mwisho ya hukumu hatutakuwa peke yetu, kwa kuwa Yesu wakili wetu, aliye pamoja na Baba , atakuwa upande wetu pamoja na watakatifu wote. Kama ilivyoandikwa, Mwana wa Mungu alitumwa duniani ili kuikomboa dunia na wale wanao mwamini hawataangamia.

Papa anasema, hukumu ya Mungu ipo katika maisha yetu ya kila siku, kulingana na jinsi tunavyotoa jibu kwa mafundisho ya Kristu na jinsi tunavyomuiga Kristu katika kuhudumia wengine, wake kwa waume wanaotuzunguka. Na hivyo ni vyema kujiandaa , kwa ajili ya kukutana na hukumu yetu tukiwa tumejaa tumaini na furaha kwa uaminifu wake Bwana.








All the contents on this site are copyrighted ©.