Mabadiliko ya sheria ya ndoa nchini Uingereza yanayotoa fursa sawa kwa ndoa za watu
wa jinsia moja, mchango wa wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye Hospitali na Magerezani
ni kati ya maeneo ambayo yanaweza kuathirika sana kutokana na uamuzi wa Serikali ya
Uingereza kuamua kubana matumizi.
Hizi ni kati
ya changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya sanjari na Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, uliofungwa rasmi wakati wa Sherehe za Kristo Mfalme wa Ulimwengu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles linasema, litaendeleza mchakato
wa Uinjilishaji Mpya kama ilivyotangazwa na Mama Kanisa ili kukabiliana na changamoto
zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na
teknolojia. Haya ni kati ya mambo yaliyojiri wakati wa mkutano wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Uingereza uliohitimishwa hivi karibuni. Maaskofu wamejadili pia umuhimu wa
Kanisa kuendelea kuwa makini ili kudhibiti vitendo vya nyanyaso za kijinsia dhidi
ya watoto wadogo.
Askofu mkuu Antonio Mennin, Balozi wa Vatican nchini Uingereza
ameshiriki pia katika mkutano huu. Maaskofu wamejadili kuhusu mashauri wanayopaswa
kupewa Mapadre wanapohudumia ndoa za watu wa jinsia moja, zilizopitishwa nchini Uingereza
na kwamba, sheria hii inatarajiwa kuanza kutumika Mwaka 2014. Kanisa Katoliki halitalazimika
kisheria kufungisha ndoa za watu wa jinsia moja na kwamba, Mapadre na watawa wanaotoa
huduma za maisha ya kiroho Hospitalini na Magerezani wataendelea na utume wao, kwani
wao wanadhamana maalum katika maisha na ustawi wa wagonjwa na wafungwa: kiroho na
kimwili.
Askofu mkuu Mennin amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza. Anawashukuru
na kuwapongeza kwa mikakati makini ya shughuli za kichungaji wanayoitekeleza nchini
Uingereza. Amewataka Maaskofu na waamini katika ujumla wao, kusimama kidete kulinda
na kudumisha misingi ya ndoa na familia kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, kwani ndoa
za watu wa jinsia moja, zina athari kubwa katika maisha na ustawi wa familia.
Kanisa
linakabiliana pia na changamoto za ufundishaji wa dini shuleni, ikiwa kama muswada
wa sheria ya kifo laini utapitishwa nchini Uingereza na hivyo kuhalalisha mtu kuwa
na haki ya kutema zawadi ya maisha. Askofu mkuu Mennin anawataka Maaskofu na waamini
katika ujumla wao, kutokatishwa tamaa na changamoto hizi bali waendelee kusimamia
kweli za Kiinjili, utu na maadili mema.
Amegusia vigezo vya kichungaji vilivyobainishwa
na Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kuwatafuta Maaskofu watarajiwa, kwani
hii ni dhamana nyeti na muhimu katika maisha na utume wa Kanisa.
Askofu mkuu
Antonio Mennin anasema ataendelea kufanya hija za kichungaji kwenye Majimbo ya Kanisa
Katoliki nchini Uingereza ili kufahamu: furaha, matumaini, kinzani, fursa na changamoto
zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa nchini Uingereza.