Siku ya haki msingi za binadamu kimataifa: UN yamkumbuka Tata Madiba!
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 10 Desemba inaadhimisha Siku ya Haki
msingi za binadamu na kwa namna ya pekee mwaka 2013, Umoja wa Mataifa unaadhimisha
Miaka 20 tangu ulipofanyika mkutano wa haki msingi za binadamu, huko Vienna Austria
na ukachangiwa na wadau mbali mbali na baadhi ya mafanikio yake yameanza kuonekana.
Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, Umoja wa Mataifa umesimama kidete
kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kwa kukazia msingi wa sheria, kwa kuwasaidia
waathirika pamoja na kuwahamasisha viongozi wa serikali kutekeleza wajibu wao msingi
pamoja na kuvishirikisha vyama vya kiraia. Lengo ni kuwajengea watu uwezo wa kutambua
na kusimamia haki zao msingi.
Ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Bwana Ban Ki-Moon,
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya haki msingi za binadamu,
dhamana ambayo ni chanzo cha kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, lakini utekelezaji wake,
lazima ujioneshe katika utashi wa kisiasa kutoka kwa nchi wanachama. Haki msingi za
binadamu zinapaswa kulindwa na kuendelezwa katika ngazi mbali mbali, ili kuzuia mauaji
ya kimbari kama yalivyojitokeza katika baadhi ya nchi pamoja na uvunjifu mkubwa wa
haki msingi za binadamu.
Umoja wa Mataifa kwa sasa umeanzisha kampeni inayopania
kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa haki msingi za binadamu; kwa kuzitambua na kuwajibika
kuzilinda na kuzitetea. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutoa jibu la haraka katika
maeneo ya uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa
wanahamasisha kutekeleza ahadi zao kwa vitendo.
Siku hii, Umoja wa Mataifa
unamkumbuka Mzee Nelson Mandela aliyesimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima
ya binadamu, haki na amani. Ataendelea kukumbukwa kuwa ni kiongozi aliyetetea haki
za binadamu kwa wote.