Guinea Bisssau Ijumaa kufunga na kusali kwa nia ya kuombea amani.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Bissau, Askofu Jose Camnate na Askofu Pedro Zilli wa
Jimbo Katoliki la Bafata katika nchi moja, wametoa mwaliko kwa waamini, Ijumaa 13
Desemba 2013, iwe ni Siku ya kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini
mwao.
Taarifa iliyopelekwa katika vyombo vya habari Katoliki, imetoa ombi hilo
la Maaskofu likiwataka Wakatoliki kusali zaidi kwa ajili ya kuombea amani na haki,
wakisema ni Mungu tu anayeweza kuingilia kati, na kuleta utulivu wa kudumu katika
taifa hilo.
Guinea-Bissau haijawahi kuwa na amani tangu kujipatia uhuru kutoka
kwa Ukoloni wa Ureno mwaka 1974. Tangu wakati huo, kumekuwa na matukio mbalimbali
ya serikali kupinduliwa na majaribio ya mapinduzi ya kijeshi. Maelfu ya watu waliuawa
na mali kuharibiwa katika mapinduzi hayo. Ukosefu wa utulivu wa kisiasa uliosababishwa
na jeshi, ni kati ya sababu kuu zinazo rudisha nyuma maendeleo ya taifa hilo hata
leo hii.