Guinea Bissau: kufunga na kusali hapo tarehe 13 Desemba 2013 ili kuombea Amani Duniani
Baraza la Maaskofu Katoliki Guinea Bissau linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kufunga na kusali hapo tarehe 13 Desemba 2013 kwa ajili ya kuombea amani duniani,
Barani Afrika na kwa namna ya pekee nchini Guinea Bissau.
Maaskofu wanapenda
kumwomba Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, maombi na mfungo ili aweze kuwakirimia ujasiri
kwa kupokea zawadi ya amani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika: ukweli,
haki na upatanisho. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, viongozi kutoka Barani Afrika
na viongozi wa Guinea Bissau hawana budi kusimama kidete kulinda na kutetea maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Wananchi wanapaswa kujikita katika
ari na moyo wa kutetea demokrasia ya kweli, utu wema, kanuni na maadili ya kazi. Viongozi,
wanasiasa na wanajeshi ambao wanadhamana ya kulinda mafao ya wengi wawe na ujasiri
wa kuonesha tunu hizi msingi katika maisha na vipaumbele vyao. Jamii zijenge na kuimarisha
mshikamano wa kimataifa.
Maaskofu wanawaalika wananchi wa Guinea Bissau hata
katika umaskini wao, kile kidogo watakachojinyima, wakikusanye kwa ajili ya kuwasaidia
wananchi wa Ufilippini, waliokumbwa na tufani, iliyosababisha maafa makubwa kwa watu
na mali zao. Kwa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Ufilippini, Baraza la Maaskofu
Katoliki Guinea Bissau limeamua kwamba, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Majilio, yaani
hapo tarehe 22 Desemba, 2013, waamini watakusanya sadaka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi
wa Ufilippini.
Maaskofu wa Guinea Bissau pamoja na waamini hivi karibuni wameadhimisha
Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwa hija na maandamano makubwa katika
Madhabahu ya Bikira Maria wa Cacheu, wakiongozwa na kauli mbiu "Pamoja na Bikira Maria
tunatembea katika Mwanga wa Imani. Hija hii imehudhuriwa na waamini wa dini na madhehebu
mbali mbali ya Kikristo kama kielelezo cha mshikamano wa dhati katika kuombea: haki,
amani na upatanisho wa kweli miongoni mwa Jamii.