2013-12-09 09:30:28

Uhuru wananchi!!


Rudisha kumbu kumbu zako miaka ile - piga picha ya kiongozi mzalendo, mtulivu, mpenda watu, ambaye siasa yake ipo kwa lengo la watu wake. Amepanda juu ya gari la zamani "Land Rover 109", mkononi ana kipaza sauti duni. Ukiangalia macho ya watu walio mkutanoni, yana nuru ya matumaini kwa kiongozi wao kana kwamba wamekutana na Bwana Yesu juu ya mwana punda.

Kiongozi anapaza sauti yake iso hata na chembe ya unafiki, ".. Uhuru Wananchi.." Wao wakijibu kwa nguvu sana hata kama majumbani kwao hawakunywa chai wala uji, "… Kazi ya TANU..". Nimekumbuka sana enzi hizo nikiwa darasa la tatu huko Kisanga, Kilosa, Mkoani Morogoro. Na hii ikaamsha sala ya kuombea viongozi wetu wa leo wanaojiangalia wao wenyewe na kusahau lengo la watu na nchi yao; yaani: mafao ya wengi, utu na ustawi wa kila mtanzania, daima wakiwa wameshibana na kushikamana kama ndugu!

Mungu ibariki Tanzania yetu na watu wake. Bariki Baba mafuta na madini yetu siku moja na sisi tuwe kama wengine ambao katika ardhi yao hujuwajalia hata tone la mafuta. Bariki na kuwanyanyua viongozi wetu kwa mkono ule ule uliowanyanyulia Musa, Yoshua, Daudi na Suleimani, wakawa ni mfano bora wa kuigwa na mataifa jirani.

Baadhi ya watanzania wanasema, Uzalendo umemezwa na ubinafsi. Hii hali inakwamisha uhuru wa kiuchumi wa nchi yetu. Ubinafsi unafanya watu wajishughulishe zaidi na maendeleo yao binafsi, tazama tembo na misitu inavyoisha, ni kwaajili ya manufaa binafsi, sijasikia hata mara moja wakisema mauzo ya vipusa na mbao yamelingizia taifa kiasi fulani, bali ni kushikwa vipusa na mininga katika mikono ya watu binafsi kwa manufaa binafsi.
Angalia mikataba, watu wanajinufaisha, hawaadibishwi zaidi ya kuwaundia ofisi nyingine. Zamani kuna waziri aliingia mkataba haramu wa manunuzi ya kivuko cha Kigamboni kwa kukosa uzalendo na kuhatarisha maisha ya wana Kigamboni, aliadibishwa kizalendo.
Kila siku ni afadhali ya jana. Sichukii maendeleo binafsi, ila yana faida gani kama wengi wanabaki maskini kati ya tajiri mmoja aliyejilimbikizia mali?Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania ni: “Vijana ni nguzo ya rasilimali watu; tuwaamini, tuwawezeshe na tuwatumie kwa manufaa ya taifa letu.”








All the contents on this site are copyrighted ©.