Nia za jumla na kimissionari za Papa kwa mwezi Desemba 2013
Nia ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Desemba ni ili kwamba, watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi waweze kupata hifadhi na kuonja upendo wa dhati.
Upendo ni
kati ya mambo muhimu sana anayohitaji manadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani,
hata watoto wanahitaji kuonjeshwa upendo na mshikamano wa dhati, unaowawajibisha wadau
mbali mbali, lakini kwa namna ya pekee dhamana hii nyeti inawagusa wazazi na walezi.
Kanisa
linatambua umuhimu wa pekee walionao wazazi na walezi katika malezi na makuzi ya watoto
wao, kwani familia ni mahali pa kwanza pa maisha ya kijamii na huduma; ni shule ya
tunu msingi za kijamii na maendeleo yake. Ustawi na maendeleo ya watoto kwa kiasi
kikubwa yanategemea sera na mikakati inayotolewa na Serikali husika, katika kuzijengea
familia uwezo wa kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa watoto mintarafu makuzi na
malezi yao.
Kuna kilio kikubwa cha watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia
wanaotafuta kuheshimiwa, kupendwa na kuthaminiwa; ili kulinda na kutetea haki zao
msingi, utu na heshima yao, tangu pale wanapotungwa mimba, hadi mauti ya kawaida yanapowafika
kadiri ya mpango wa Mungu, bila kuangalia hali ya mtoto kama ni mzima au ana ulemavu,
wote ni zawadi kutoka kwa Mungu. Watoto hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa mfano
wa Mungu. Vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na mwelekeo huu, havithamini haki msingi
za watoto. Matendo adili yasaidie mchakato wa kulinda na kudumisha haki msingi za
watoto sehemu mbali mbali za dunia.
Nia za kimissionari za Baba Mtakatifu Francisko
kwa mwezi Desemba ni ili kwamba, Wakristo wakiangazwa na Neno wa Mungu aliyefanyika
mwili, waweze kuwaandaa walimwengu kwa ajili ya ujio wa Mkombozi. Waamini wanaalikwa
kwa namna ya pekee, kujiandaa kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo mema
kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo Masiha. Wahusika wakuu ambao ni Zakaria na Elizabeth,
wachungaji wa kondeni, Mamajusi, watu wa kawaida lakini kwa namna ya pekee, Bikira
Maria na Mtakatifu Yosefu wawe ni mfano bora wa kuigwa katika kipindi hiki cha Majilio!
Hawa ni wale walioguswa kwa namna ya pekee na maandalizi ya ujio wa Masiaha.
Jambo
la kujiuliza, Je, walimwengu wa nyakati hizi wanaonesha ari na mwamko wa kumngoja
Masiha ili aweze kuzaliwa tena katika maisha yao? Pengine wanamwona kuwa ni kizingiti
katika mikakati ya maisha yao? Mwelekeo huu upo pia kwa baadhi ya waamini wanaotaka
njia ya mkato ili kufikia furaha. Licha ya mapungufu na majanga ya maisha, lakini
bado watu wana kiu ya kutaka kukutana na Kristo, ili aweze kuleta magezi katika ulimwengu
mamboleo. Haijalishi hata leo kusikia manabii wanaotangaza ukombozi wa chapu chapu
lakini baadaye waamini wanajikuta wakichanganyikiwa na kukata tamaa ya maisha na hivyo
hija ya Imani yao inaingiwa mchanga!
Yesu Kristo aliyezaliwa katika hali ya
umaskini ni kielelezo kwamba, Yeye ndiye anayeweza kuzima kiu ya furaha na amani katika
maisha ya mwanadamu. Kipindi cha Majilio, kiwe ni msaada kwa Waamini kujivika utu
mpya kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu na Matendo ya huruma kwa jirani.
Waamini wajiandae kikamilifu wasijekujikuta Yesu anawafikia wakiwa bado wamemezwa
na malimwengu. Waamini waandae mioyo na familia zao ili Kristo aweze kuzaliwa katika
mazingira ya: Imani, Mapendo na Matumaini; Amani na mshikamano wa dhati kwa maskini
na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii: kiroho na kimwili.