2013-12-09 08:36:44

Msianze kujenga familia kabla ya kuitikia wito wa ndoa!


Tumsifu Yesu Kristo…!
Mpendwa Msikilizaji wa wa Radio Vatican, katika kipindi chetu kilichoopita, tulitazama kwa ufupi utangulizi wa jumla wa kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, ambamo tunayaangazia maisha ya Ndoa na Familia. RealAudioMP3
Leo tunaangazia kwa ufupi juu ya umuhimu wa maandalizi katika kuuitikia wito wa ndoa na kuingia katika maisha ya familia. Kwetu sisi Wakristo Maisha ya ndoa ni WITO. Ni Mungu mwenyewe anawaita wanadamu katika miito mbalimbali. Na kuitikia ainayoyote ya wito ni kufanya maamuzi mazito ya maisha. Hali kadhalika, Kuingia katika ndoa ni kufanya MAAMUZI MAZITO YA MAISHA.

Maamuzi hayo yana nguvu ya kimaadili na nguvu ya kisheria. Ni uamuzi-msingi ambao mtu huufanya mara moja kwa maisha yote. Ndiyo maana taratibu-Kanuni za Kanisa letu zimeweka umri na vigezo vya mtu kuweza kuitikia wito huu wa ndoa na familia. Japo ni haki ya kila mtu kuoa au kuolewa, lakini sheria ya Kanisa inaratibisha haki hiyo; inatuelekeza ni umri gani mtu anaweza kuoa au kuolewa; na vigezo gani vinamhalalisha mtu kuoa au kuolewa. Kanisa linaamini kuwa ni katika umri huo mtu anaweza kufikiri na kuelewa vema na kufanya maamuzi sahihi katika maisha yake mwenyewe; na pia anaweza kuhimili majukumu mbalimbali ya maisha ya ndoa na familia.

Maisha ya ndoa ni maisha ya mahusiano. Kwako unayeitikia wito wa ndoa, ni maisha yenye kuleta mabadiliko katika maisha yako yote. Utajipatia mabadiliko binafsi, hautakuwa na uhuru wa nafsi kama ambavyo haukuwa katika wito wa ndoa. Utajiletea pia mabadiliko ya kijamii, utaitwa mama fulani, mke wa fulani au baba fulani. Ni maisha yanayokwenda kubadili hata mfumo wako wa kufikiri, yaani badala ya kubaki katika ulimwengu wa mimi, unaingia katika ulimwengu wa sisi, au mimi na mwenzangu, mimi na familia yangu. Hapa ndipo ile hali ya mwanadamu kama ki-umbe jamii inapodhihirika wazi zaidi na zaidi.

Kuupokea wito na maisha ya ndoa, ni kukubali kuishi katika ulimwengu wa mwingine na kuwa tayari mwingine (yaani mwenzi wako tu) kuingia katika ulimwengu wako. Na kwa namna hiyo, ni kukubali kushirikishana uhuru wa nafsi. Na kwa namna ya juu kabisa, wito na maisha ya ndoa hujenga umoja wa nafsi hizo mbili zinazoletwa pamoja kwa upendo wa kweli. Neno linasema, “Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena bali mwili mmoja.” [Mk. 10:8].

Kumbe, mpendwa msikilizaji, kwa vile ni maisha yenye kuleta mabadiliko kwa wahusika na kwa jamii nzima, NI VEMA KUFANYA MAANDALIZI YA KUTOSHA. Kwa vile tunaitazama familia kama Kanisa la nyumbani; kwa mwangwi wa Kanisa lenye asili katika Utatu Mtakatifu [Rej. Yoh 1:1-14); tunapenda pia maandalizi yetu katika kupokea wito wa ndoa na kulijenga Kanisa la nyumbani, tuyaweke katika utatu. Sehemu ya kwanza ni waoanaji wenyewe; sehemu ya pili ni jamii inayowazunguka, zikiwemo na familia wanamotoka waonaji hawa, sehemu ya tatu ni MUNGU.

Tuiangazie kwanza sehemu hiyo ya tatu YAANI UHUSIKA WA MUNGU. Hapa tunataka kusema hivi: Wewe unayejiandaa kuitikia wito wa ndoa, tangu mwanzo kabisa mhusishe MUNGU. Ni Mungu ndiye anayepanda mbegu njema ya upendo ndani ya waonaji. Upendo wa kweli haununuliwi kwa fedha au vitu au umaarufu. Mchumba mwema, ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mchumba mwema hapatikani kwenye disko wala kilabuni. Mchumba mwema, ambaye baadaye atakuwa mume mwema au mke mwema, hutoka kwa Mungu.

Kwa wewe ambaye unajiandaa kuitikia wito wa ndoa, ni vema kusali kwa machozi na kite na imani timilifu kumwomba Mungu akujaalie kupata mchumba mwema. Na kisha kumpata huyo, ni kuendelea kumwombea ili yule mwovu asianze kuwapepeta tangu mwanzo. Na baada ya kuingia katika maisha ya Kanisa la nyumbani, kila mmoja azingatie UTUME WA KUMWOMBEA MWENZI WA NDOA. Si mara chache, wanandoa wanasahau kuombeana kwa Mungu. WENGI WANAKUMBUKA KUSEMANA-SEMANA, KUTUKANANA, KUAIBISHANA NA KUANIKANA MITAANI kuliko kuombeana, kuwekana mikononi mwa Mungu. Kuombeana kwa Mungu ni tunu kubwa sana (Rej. Sala ya Tobia akimwombea mkewe na agano lao. [Tob. 8:4-7]. Mungu ahusishwe katika maisha mazima ya Kanisa la Nyumbani.

Sehemu ya pili, tukumbuke kuhusishwa kwa jamii. Katika nyakati zetu hizi, pamoja na changamoto mbalimbali zinazotuzunguka, tusisahau kwamba wito wa ndoa na maisha ya familia ni suala la kijamii. Mazingira ya nyakati zilizopita yaliruhusu kwa uwazi zaidi jamii nzima kushirikishwa katika maandalizi ya mtu kuingia katika maisha ya ndoa na familia. Leo hii ni kama jamii na hata familia pengine haishiriki kwa undani zaidi, zaidi ya kukusanya michango na kuandaa sherehe za harusi. Hapa ni juu yetu kufikiri, NI NAMNA GANI TUWASAIDIE VIJANA WETU ILI KATIKA MAANDALIZI NA WAKATI WA UCHUMBA WASIJIFANYIE MAKOSA YATAKAYOWATESA MAISHA YAO YOTE. Wazazi tusipokuwa macho katika hilo; adhabu yetu itakuwa ni kutunza watoto wa watoto wetu.

Siku chache zilizopita, uchumba uliheshimika na ilikuwa ni hatua muhimu katika maandalizi. Lakini polepole kwa walio wengi uchumba unafifishwa; wanaanza kujenga familia kabla ya kuitikia wito wa ndoa. Matokeo yake, ni kama wageni wawili wasiofahamiana wanaanza kuishi pamoja, baada ya siku chache wanaamua kufunga ndoa, na kwa sababu walianza kuishi pamoja bila kufahamiana vizuri wanafunga ndoa wakiwa tayari wamechoka na maisha ya ndoa.

Hiyo ni moja ya siri za ndoa changa nyingi kupoteza mwelekeo na kuvunjia mapema mno pamoja na ufahari na umaridadi wa sherehe zile za harusi. Hilo linaleta maumivu kwa Kanisa na kwa jamii kwa ujumla.

Tunazidi kumwomba Mungu mwingi wa huruma na mwasisi wa agano la ndoa, aziimarishe ndoa zote ili Kanisa liendelee kujipatia watoto wengi zaidi wa Ufalme. Yeye mwenyewe awape vijana na watu wote ujasiri wa kuwa tayari kuitikia wito wa ndoa ili kulijenga Kanisa la nyumbani linalofurahi, Kanisa la nyumani lililo matumaini ya mwanadamu. Hadi kipindi kijacho, kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.