2013-12-09 08:53:40

Barua ya kichungaji kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe


Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika barua yake ya kichungaji iliyotolewa hivi karibuni linasema, nchi ya Zimbabwe inakwenda mrama kuliko hata ilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu, uliompatia ushindi wa kishindo Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Hali ya maisha ya wananchi wengi inaendelea kudorora, kiasi cha kuweka rehani tunu msingi za haki, amani na usalama wa raia.

Wananchi wa Zimbabwe wanaendelea kukata tamaa kutokana na ukata wa maisha na hakuna juhudi za makusudi zinazofanywa na Serikali iliyoko madarakani ili kurekebisha hali hii. Huduma za elimu, afya, maji safi na salama pamoja na miundo mbinu ni mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa kwa haraka kwani hali ni mbaya, kuliko inayodhaniwa na wengi! Mgawo wa maji na umeme umekuwa ni wimbo wa kawaida kwa wananchi wa Zimbabwe, hali ambayo inakwamisha maendeleo endelevu na jitihada za wananchi kujikwamua kutoka kwenye umaskini wa hali na kipato.

Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe katika barua yake ya kichungaji linasema kwamba, kuna haja kwa Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo kuwa na sera na mbinu mkakati utakaorekebisha huduma katika sekta ya elimu, afya, maji, nishati na usafirishaji. Zimbabwe ianze tena mchakato wa ujenzi wa uhusiano wa kimataifa, ili kusaidia marekebisho ya kiuchumi, kwa kuwa na soko lenye uhakika pamoja na kuirudishia Zimbabwe hadhi yake ya kuwa ni mzalishaji mkuu wa mazao ya chakula na biashara kusini mwa Afrika, ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa watu wengi Zaidi!

Maaskofu Katoliki Zimbabwe wanasema, viwanda vimebaki kuwa ni magofu na maficho ya makundi ya wahuni na majambazi. Utu na heshima ya wananchi wa Zimbabwe inashushwa kwa kuuziwa bidhaa hafifu zisizo na ubora wala viwango. Uchaguzi mkuu wa Mwezi Julai, 2013, uliohitimisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwa imeundwa baada ya kinzani za uchaguzi mkuu wa Mwaka 2008, haujaonesha matumaini waliyokuwa nayo wananchi wa Zimbabwe.

Umaskini wa hali na kipato umeongezeka, wananchi wengi wanalazimika kwenda kuhemea katika nchi za jirani hata kwa mambo ya kawaida kabisa! Ushirikiano kati ya vyama vya kisiasa kwa ajili ya mafao ya wengi, unaonekana kutoweka kabisa! Maaskofu wanawahamasisha wanasiasa nchini Zimbabwe kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya kutetea: haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Zimbabwe ni kati ya nchi chache za Kiafrika zilizobahatika kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali na mali asili; Watu wanaomcha Mungu; wenye ujuzi na maarifa; mambo yote haya yakitumiwa vyema yanaweza kuleta mwamko mpya wa maendeleo na ubora wa maisha kwa wananchi wengi wa Zimbabwe.

Kuna haja kwa wanasiasa kuwa na utashi wa kisiasa, ili kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Maaskofu wanawaalika wadau mbali mbali kujifunga kibwebwe ili kushirikiana na kushikamana kwa pamoja kwa ajili ya kutunga sera na mikakati ya maendeleo katika sekta mbali mbali za maisha ya wananchi wa Zimbabwe na utengemanano wa Kikanda na katika Jumuiya ya Kimataifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.