2013-12-07 08:03:17

Wito? Yataka moyo!


Mheshimiwa Padre Vito Nardini, Mkuu wa Shirika la Mapendo, maarufu kama Warosmini, tarehe 9 Desemba 2013 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Nadhiri za daima kwa wanashirika wake wafuatao: Justus Okibo, kutoka Kenya, Aji Alphonce kutoka India pamoja na Aristid Shayo kutoka Tanzania. Ifuatayo ni historia fupi ya safari ya wito wa Frt. Aristid Shayo katika mahojiano maalum na Radio Vatican. RealAudioMP3
Naitwa Frateri Aristid Shayo. Nilizaliwa katika jimbo la Moshi parokia ya Lowerere. Mimi ni mtoto wa pili kati ya watoto 9 wa Mzee Michael Shayo na Rosalia Makombo. Tangu utoto wangu, nimelelewa katika maadili na desturi za kikatoliki. Kila siku asubuhi na jioni ilikuwa ni sheria kusali pamoja katika familia yetu. Nikiwa mtoto niliwahi kusinzia wakati wa sala ya siku ila mama yangu alikuwa akinimwagia maji ya baridi ili niwe macho na kushiriki katika sala. Sala ya kwanza kabisa kujifunza katika utoto wangu ilikuwa sala ya kubariki chakula na kushukuru ambayo nilifundishwa na mama yangu.
Historia fupi ya wito wangu! Yataka moyo!
Katika utoto wangu, nilitamani sana kutumikia misa. Kwa kifupi ni kwamba nilikuwa navutiwa sana na kutoa huduma pale altareni hasa kushika chetezo. Kwa kweli sikuwa naelewa ni kwa nini hasa nilivutiwa hivyo ila nilitamani kufanya hivyo muda na wakati wowote. Nilitamani sana siku moja na mimi nifanye kama anavyofanya Padre altareni. Hii ilinifanya nitamani kuingia seminarini. Nilipomaliza shule ya msingi niliomba kujiunga na Seminari ndogo ya Maua, iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi lakini kwa bahati mbaya sikuweza kuchaguliwa. Hii ilinifanya nikate tamaa kabisa.
Niliamua kutokupoteza muda na kuendelea na masomo ya sekondari, nilisoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika sekondari ya kutwa ya Tarakea kule Rombo, Kilimanjaro. Muda wote nikiwa shuleni hapo nilikuwa najishughulisha na shughuli za TYCS lakini wazo la kujiunga na seminari halikuwepo tena moyoni. Baada ya kidato cha nne, nilijiunga na kidato cha tano katika sekondari ya Galanos kule mkoani Tanga. Hapa ndipo palikuwa kitovu cha kugundua tena wito wangu. Kama kawaida nilijishughulisha sana na shughuli za kanisa shuleni pale hasa katika chama cha wanafunzi wakatoliki Tanzania (TYCS).
Mara kwa mara Padre Titus Mdoe ambaye kwa sasa ni makamu askofu wa jimbo kuu la Dar es Salaam alikuwa anatutembelea. Akiwa kama mlezi wa vijana jimboni Tanga alitulea kwa namna ya kipekee katika imani katoliki. Zaidi sana Padre Firmati Tarimo ambaye kwa sasa ni mkuu wa Warosmini kanda ya Afrika alikuwa anatutembelea pia pale shuleni.
Siku ya siku mashirika matano ya kitawa na kimisionari yalifanya semina ya kukuza miito katika makao makuu ya Warosmini Mwambani Tanga. Walikuwemo Warosmini wenyewe, Wayesuit, Mamisionari wa Afrika, Wadomenikani na ”Christian Brothers”. Tulienda mwambani kuwasikiliza kuanzia Ijumaa jioni hadi Jumapili. Kwa kweli hapo ndipo nilipogundua tena wito wangu. Kuanzia siku hiyo nilifanya maamuzi ya kuwaza tena kuhusu maisha ya kipadre. Niseme tu kwamba, nilivutiwa sana na karama ya Mwenye heri Antonio Rosmini ambayo ni Mapendo yasiyo na kikomo kwa Mungu na kwa Jirani.
Nilijiunga na Shirika mwaka 2004, malezi ya kwanza nilifanyia Lushoto, baadaye, nikasoma Falsafa Nairobi Kenya. Kwa sasa nipo hapa Roma nasoma Teologia mwaka wa pili katika chuo kikuu cha Kipapa cha Lateran. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa kunipa nguvu hadi nikaweza kudumu katika safari hii. Nazidi kumuomba neema zake ili niweze kusonga mbele hadi mwisho. Nawashukuru wazazi wangu kwa kunilea katika maisha ya kikatoliki.
Nawashukuru Warosmini wote kwa kunipokea na kunilea katika Shirika hili la Mapendo. Tarehe 9-12-2013, ni siku ya muhimu sana kwangu kwa sabubu pamoja na kufunga nadhiri za daima, watanzania wote tunasheherekea uhuru wetu. Kwa namna ya pekee naiombea nchi yetu amani ya kweli na ya kudumu. Ninawaomba mnisindikize katika safari hii ya maisha ya kitawa, ili kweli niweze kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa!
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.