2013-12-07 15:33:28

Utu na heshima ya mwanadamu vipewe kipaumbele cha kwanza!


Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni ukweli wa kimaadili ambao ni chanzo cha maisha ya binadamu, lakini katika ulimwengu wa utandawazi, kuna baadhi ya makundi ya watu yanayotaka kujenga na kudumisha utamaduni usiojali wala kuthamini utu na heshima ya binadamu, jambo ambalo kwa baadhi ya watu linaanza kuwa ni la kawaida!

Matokeo ya utamaduni huu ni uzalishaji wa kundi kubwa la maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii na kwamba, Mwenyezi Mungu hana nafasi tena katika mipango na vipaumbele vya mwanadamu. Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 7 Desemba 2013, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Utu wa Mwanadamu; "Dignitatis Humanae".

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuamsha dhamiri zao nyofu, huku wakiongozwa na Neno la Mungu, ili waweze kuamua na kutenda; kupanga na kuchagua ni mambo yepi yanayopaswa kubadilishwa! Neno la Mungu linawahamasisha watu kusimama kidete kulinda na kutetea maisha na utu wa kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na mwanadamu ni muhimu sana katika hija ya Watu wa Mungu hapa duniani, ili kulinda na kutetea uhuru wa kidini, tayari kutangaza Injili ya Uhai katika hatua zake zote; haki ya kuwa na fursa za ajira nzuri, familia na elimu bora.

Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe hawa kutokana na mchango wao unaopania pamoja na mambo mengine kuwasaidia watu, jumuiya na taasisi kutambua kanuni maadili kuhusu utu wa binadamu kuwa ni kiini cha uhuru wa kweli na haki. Ili kufanikisha dhamana hii kuna haja ya kuendeleza majiundo makini kwa waamini walei kutoka medani mbali mbali za maisha, hasa wanasiasa ili waweze kufikiri na kutenda kadiri ya Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Waamini walei watekeleze nyajibu zao kwa njia ya majadiliano, wakishirikiana na wengine katika misingi ya ukweli, uaminifu wa kiakili; kwa kushirikishana kama si imani basi mwono wa mtu na jamii inayowazunguka sanjari na matokeo yake kimaadili. Mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza.








All the contents on this site are copyrighted ©.