Ulimwengu wa digitali unakumbatia hali halisi ya maisha!
Kumtangaza Kristo katika nyakati hizi za dijitali ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Maadhimisho
ya ishirini na sita ya Mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei, ulioanza
hapo tarehe 5 Desemba 2013 na kuhitimishwa rasmi tarehe 7 Desemba 2013 hapa mjini
Vatican.
Wajumbe katika mkutano huu wameangalia kwa kina na mapana, maendeleo
ya sayansi na teknolojia ya habari fursa na changamoto zake katika kufunga sehemu
ya kwanza ya Karne ya ishirini na moja hasa katika matumizi ya mitandao ya kijamii,
ambayo watumiaji wake wakuu kimsingi ni waamini walei.
Ni jukumu la Mama Kanisa
kuhakikisha kwamba, anaongeza juhudi, bidii na maarifa ya kuwatangazia Habari Njema
ya Wokovu wale wanaoishi katika ulimwengu wa dijitali, ili waweze kuonja Injili ya
Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Mitandao ya kijamii inatumika
katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, kumbe Kanisa linapaswa kuifahamu
vyema ili kuwafikia watumiaji wake.
Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza
la Kipapa la Walei anasema kwamba, watumiaji wa mitandao ya kijamii wengi wao ni vijana.
Mitandao ya kijamii iwasaidie vijana kugundua fursa zilizopo na athari zake, ili waweze
kuwa makini, wasijekujikuta wanatumbukizwa kwenye "majanga ya maisha". Kanisa haliwezi
kujiweka pembeni na kuwa mtazamaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii, lazima lijiingize
huko kwani, "utamu wa ngoma, ni kucheza" ndivyo wanavyosema Waswahili.
Professa
Mario Pollo mmoja kati ya wawezeshaji wakati wa mkutano huu anasema kwamba, maendeleo
ya sayansi na teknolojia ya habari yamemsaidia mwanadamu kupiga hatua kubwa ya maendeleo
katika nyanja za mawasiliano ya kijamii, kiasi hata cha kubadili mfumo na mtndo wa
maisha. Haya ni mawasiliano yanayosambaa kwa kasi ya ajabu, kiasi kwamba, muda si
tatizo tena, kiasi kwamba zile Jamii ambazo zilizoea mawasiliano ya zawani zinajikuta
zikichechemea ili kukabiliana na kasi na wingi wa habari unaotolewa.
Kwa upande
wake, Professa Tonino Cantelmi amesema kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia
ya habari yamemwezesha mwanadamu kuwa na mwono mpya wa mahusiano yake na watu wengine.
Amewataka wajumbe kutambua nguvu, fursa na athari zinazoweza kupatikana kutokana na
maendeleo haya katika maisha ya mwanadamu. Watu wanapaswa kujifunza kuwa na matumizi
sahihi ya mitandao ya kijamii.
Professa Antonio Spadaro amewakumbusha wajumbe
kwamba, ulimwengu wa digitali si wa kufikirika tu au unaoelea kwenye "Ombwe", bali
ni sehemu ya ukweli wa maisha ya kila siku unaowagusa wengi, lakini kwa namna ya pekee
vijana wa kizazi kipya. Kumbe, Mama Kanisa anawajibu wa kuwasaidia vijana kutambua
fursa zinazoweza kupatikana kwenye mitandao ya kijamii sanjari na kung'amua athari
zake, ili mitandao ya kijamii liwe ni Jukwaa jipya la Uinjilishaji kwa watu wanaoishi
kwenye ulimwengu wa dijitali.
Huu ni ulimwengu unaokumbatia hali halisi ya
maisha. Watumiaji wa mitandao wasijifungie tu huko, bali wanapaswa kutoka ili kujenga
na kuimarisha mahusiano ya kijamii katika hali halisi ya maisha!