Nchi za Kiafrika kuendeleza ushirikiano wa karibu na Ufaransa
Ufaransa inaunga mkono juhudi zinazofanywa na nchi mbalimbali dhidi ya ujangili duniani
kwani ujangili unaleta madhara makubwa kiuchumi, kiusalama na kimazingira. Rais wa
Ufaransa Francois Hollande amesema hayo katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika
zinazokutana jijini Paris kujadili tishio la tembo na wanyama walio katika hatari
ya kutoweka duniani. Mkutano huo umefanyika tarehe 5 Desemba, jioni katika Hotel
de la Marine, mjini Paris. Rais Jakaya Kikwete anahudhuria kikao hicho pamoja na viongozi
wengine wakuu kutoka bara la Afrika. "Ufaransa iko tayari kushirikiana nanyi katika
vita hii, tunahitajika kuchukua hatua dhidi ya ujangili na usafirishaji wa bidhaa
zinazotokana na ujangili" amesema. Amesema tafiti zinaonesha kuwa katika kipindi
cha miaka 10 ijayo, kama kasi ya ujangili iliyoko sasa itaendelea, basi kuna hatari
ya kupoteza moja ya tano ya tembo waliopo afrika na hasa Afrika ya Kati. "Ujangili
ni tishio kubwa barani Afrika ni tishio kwa uchumi, tishio kwa usalama na pia kwa
mazimgira, lazima tukomeshe ujangili na Ufaransa imeazimia kuchukua hatua"Amesema. Amesema
Ufaransa itaweka adhabu kali kwa makosa ya ujangili na kupiga marufuku biashara ya
wanyama walio katika hatari na kwamba meno ya tembo yatakayokamatwa yataharibiwa kabisa.
"Nataka ufaransa iwe mfano katika nchi za ulaya lakini na nchi za ki-Afrika lazma
zichukue hatua kali na Ufaransa itashirikiana nanyi" Rais Hollande amesema. Akichangia
katika kikao cha viongozi wa Afrika, Rais Kikwete amezitaka nchi za kiafrika kujenga
uwezo wa kupigana na ujangili na biashara ya tembo na kuzitaka nchi za kiafrika kuungana
kuhakikisha biashara ya meno ya tembo inapigwa marufuku na masoko yake kufungwa.
Mapema akihutubia katika kikao kuhusu uchumi baina ya Afrika -Ufaransa, Rais Kikwete
amewaeleza wafanyabiashara wa Ufaransa kuwa bara la Afrika lina vigezo vyote vya kuwa
na uchumi unaovuma duniani. Amesema Afrika imejaliwa kuwa na maliasili nyingi kama
ardhi, madini, mafuta, gesi, misitu na maliasili za baharini ambavyo vingi havijaendelezwa
ipasavyo , na hii ina maanisha kuwa kuna nafasi nzuri barani humo. Amesema ili kufanikisha
ukuaji huo "Afrika inahitaji ushirikiano na Ufaransa na nchi zingine kutoka nchi zinazoendelea
na zilizoendelea kuzitumia maliasili hizi kwa ajili ya maendeleoā€¯.