2013-12-07 09:23:44

Kanisa linaukumbuka mchango wa Tata Madiba katika mchakato wa upatanisho, haki na amani!


Viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani katika salam zao za rambi rambi kwa wananchi wa Afrika ya Kusini, wamemsifu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95, kuwa ni kati ya watu walioacha mfano wa kuigwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika Karne ya ishirini na moja.

Ni kiongozi aliyesimamia kweli za maisha, akatetea haki na amani na kuhakikisha kwamba, demokrasi inapatikana na ubaguzi wa rangi unatokomezwa nchini Afrika ya Kusini. Ni kiongozi na mpigania haki ambaye alijikita zaidi katika majadiliano kama njia ya kufikia amani ya kweli badala ya kutumia silaha. Kwa miaka 27 akatupwa kizuizini, hadi alipoachiliwa huru kunako mwaka 1990, mchango mkubwa wa Kampeni ya Kimataifa. Mwaka 1993 akapewa tuzo ya amani duniani na kugawana na mpinzani wake Bwana Frederick W. de Klerk, watu ambao wameandika historia mpya ya Afrika ya Kusini.

Tata Madiba alipochaguliwa kuwaongoza wananchi wa Afrika ya Kusini, akataka kuona: utawala wa sheria na kwamba, ubaguzi wa rangi ulikuwa hauna tena nafasi kwa wananchi wa Afrika ya Kusini, bali wote kujitambua kwamba, ni wananchi wanaotegemeana na kusaidiana katika medani mbali mbali za maisha, kwa kuheshimu utu wa kila mtu na wala si rangi ya ngozi! Kila mtu akapata nafasi ya kushiriki maisha katika Afrika ya Kusini huru na mpya zaidi.

Kama Rais wa kwanza mzalendo, akagundua umuhimu wa upatanisho kama njia ya kuponya makovu ya chuki na ubaguzi wa rangi na kwamba, upatanisho ndiyo iliyokuwa njia pekee ya kudumisha misingi ya haki na amani ya kudumu. Watu wakapewa fursa ya kutubu na kuomba msamaha; ukweli ukafahamika na watu wakawa huru! Ndiyo maana watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaomboleza kwa kifo cha Mzee Madiba, mtu wa watu, liyeteseka kifungoni kwa miaka 27 na amevumilia pia mateso ya ugonjwa wake, hadi mauti yalipomfika hapo tarehe 5 Desemba 2013.

Hakuona kwamba uongozi ni kitu cha kung'ang'ania sana, akaamua kwa utashi wake kamili kung'atuka kutoka madarakani, viongozi wengine wakaendeleza pale aklipoachia Mzee Nelson Mandela. Apumzike kwa amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.