Kampeni ya Kimataifa dhidi ya baa la njaa duniani!
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaunga mkono kampeni ya Shirikisho la Mashirika
ya MIsaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika mapambano
dhidi ya baa la njaa duniani.
Kilele cha kampeni hii ni hapo tarehe 10 Desemba,
2013, Siku ya Kimataifa ya Haki Msingi za Binadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada
kwa takribani miaka 45 limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kusaidia maendeleo
endelevu katika nchi changa zaidi duniani, kwa kushirikiana na Caritas Internationalis.
Lengo ni kuendelea kuhimiza wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba
wanachukua hatua madhubuti na sera makini zitakazosaidia kupambana na baa la njaa
duniani; kwa kuheshimu haki ya mtu kupata chakula bora na hasa zaidi chakula kinachozalishwa
katika maeneo yake.
Mshikamano wa sala utafanyika kwenye Parokia na shule na
taasisi mbali mbali zinazoendeshwa na kumilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada.
Mshikamano huu unaoneshwa pia na waamini katika sehemu nyingine za dunia. Ni matumaini
ya Caritas Internationalis kwamba, kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa unaozingatia
kanuni auni, inawezekana kwa Jumuiya ya Kimataifa kutokomeza baa la njaa na utapiamlo
ifikapo mwaka 2025.
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, kila
mtu anahishi maisha yenye hadhi, bila kusumbuliwa na baa la njaa na utapiamlo; wala
wasiwasi wa ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula wala watoto kukumbwa na utapiamlo
wa kutisha unaohatarisha makuzi na maisha yao kwa sasa na kwa siku za usoni!