Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana hivi karibuni limehitimisha mkutano wake mkuu wa
Mwaka kwa kuwashukuru watu wa Mungu nchini humo kwa kufanikisha uchaguzi mkuu kwa
amani na utulivu. Uinjilishaji mpya kama njia ya kutangaza imani ya Kikristo nchini
Ghana ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana.
Hata baada
ya kusherehekea miaka 500 ya Ukristo nchini Ghana, Mama Kanisa bado anaona haja ya
kuzamisha mizizi ya imani katika maisha na vipaumbele vya wananchi wa Ghana. Uinjilishaji
mpya kama lengo la jumla, unapania kumwezesha mwanadamu kukutana na Mwenyezi Mungu,
chemchemi ya uzima na amani kwa njia ya yesu Kristo. Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa
kipaumbele cha kwanza, utu na heshima ya mwanadamu vikiheshimiwa na kuthaminiwa. Waamini
wanaalikwa kuishuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya vitendo.
Maaskofu
wanasema, Ghana watu wana mwamko wa imani, amani na demokrasia na kwamba, kuna ushiriki
mkubwa katika maisha ya kidini hali inayojionesha hata miongoni mwa wanasiasa. Pamoja
na cheche hizi za mafanikio, baadhi ya watu wanaanzaa kupata ukakasi na ubaridi wa
Injili, kiasi cha kutojisikia tena kwamba, wanachangamotishwa kujitosa kimasomaso
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo kila jumapili wanajaza Makanisa, lakini
bado hawajaonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha yao ya hadhara wanasema
Maaskofu.
Uinjilishaji mpya hauna budi kugusa roho ya mtu, ili aweze kutubu
na kumwongokea Mungu, huku akikumbatia utakatifu wa maisha. Hii ni changamoto endelevu
kwa Familia yote ya Mungu nchini Ghana. Maaskofu wanasema, kuna mila, tamaduni na
desturi njema; maisha adili; upendo kwa Mungu na jirani; ukarimu kwa jirani; dhana
ya kupenda na kuheshimu uhai; mambo yote haya ni msingi thabiti wa imani unaoweza
kusaidia mchakato wa waamini nchini Ghana kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa mataifa.
Maaskofu
wanasema, Familia ni kati ya taasisi zinazohitaji kuinjilishwa kwani inakumbana na
changamoto nyingi za maisha, ili iweze kutekeleza wajibu na majukumu yake kadiri ya
mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia hazina budi
kulindwa na kutetewa na Serikali na kwamba, hili ni jukwaa makini la Uinjilishaji.
Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa kuvihusisha vyama vya kitume kwa ajili ya familia.
Wazazi na walezi watekeleze dhamana yao kwa uaminifu na uadilifu, kwa kutambua kwamba,
wao ni vyombo vya kwanza kwa urithishaji wa tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili
na kiimani. Wawe ni ya chachu uchaji wa Mungu, ukweli, uaminifu na wachapa kazi; tunu
zinazopaswa kujionesha tangu katika maisha ya kifamilia.
Maaskofu wanawaalika
waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Ghana kusimama kidete kulinda na kutetea
misingi ya haki, amani na utulivu; waendelee kuwa ni wadau na watetezi wa mazingira.
Wapinge rushwa na ufisadi kwa matendo, wasimamie haki na mafao ya wengi pamoja na
kutunza ardhi kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho! Wanasiasa watekeleze wito
na wajibu wao kwa kuongozwa na tunu msingi za Kiinjili, daima wakijitahidi kuwa kweli
ni mfano wa kuigwa.
Maaskofu wanakazia Uinjilishaji unaokwenda sanjari na katekesi
ya kina. Biblia, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii
ya Kanisa na Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni nyenzo muhimu sana katika
azma ya Uinjilishaji kwa watu wa kizazi kipya. Waamini na watu wenye mapenzi mema,
waendelee kuchota utajiri kutoka katika nyaraka hizi sanjari na kujikita katika mchakato
wa utamadunisho.
Wananchi wa Ghana wasimezwe na malimwengu kwa kupenda sana
mali na madaraka, mambo yanayopelekea rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Rushwa imeenea
katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Ghana! Watu wakatae kutoa na kupokea
rushwa kwani ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Maaskofu wanahimiza Serikali
na vyombo husika kuhakikisha kwamba, vinatekeleza wajibu wake barabara!
Baraza
la Maaskofu Katoliki Ghana linakemea vikali ukabila na udini unaohatarisha umoja na
mshikamano wa kitaifa na wanasema kwamba, tofauti hizi ni kielelezo cha utajiri wa
wananchi wa Ghana na kamwe yasiwe ni mambo yanayowaga na kuwasambaratisha wananchi
wa Ghana. Mwishoni, Maaskofu wanawaalika waamini kujenga na kuimarisha ari na moyo
wa sala, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya.