Acheni uchafuzi wa mazingira na ukataji ovyo wa kuni!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ametoa mwezi mmoja kwa Baraza la Taifa la Mazingira
(NEMC) iwe imetoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu matumizi ya maji machafu yanayotokea
kwenye viwanda vinne vya ngozi, magunia, nguo na maturubali (canvas).
Ametoa
agizo hilo Jumamosi, Desemba 7, 2013 mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye
kiwanda cha nguo cha 21st Century kilichopo eneo la Kihonda Viwandani nje
kidogo ya mji wa Morogoro.
Akizungumza na uongozi wa mkoa, wilaya, kiwanda
hicho pamoja na NEMC ya mara baada ya kutembelea eneo ambalo limeathirika na maji
yanayotiririka kutoka kwenye viwanda hivyo, Waziri Mkuu alisema tatizo lililopo linachangiwa
na kutokuwepo kwa mtu au taasisi maalum ya kusimamia mabwawa ya mfumo wa majitaka
(waste management ponds).
“Viwanda hivi vilibinafsishwa lakini mfumo wa usafishaji
majitaka haukubinafsishwa... NEMC iishauri Serikali nini kinapaswa kifanyike. Ifanye
utafiti kuhusu matumizi ya majitaka yanayotoka kwenye viwanda hivi na ilete uchambuzi
huo Serikalini,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye alitembelea eneo la Kihonda Mbuyuni
katika kata ya Mafisi ambako maji hayo yanaingia korongoni na kuelekea mto Ngerengere,
alishuhudia mifereja ya maji machafu yenye harufu kali na rangi mchanganyiko ya kijani
na bluu ikitiririka katikati ya nyumba za watu.
“Hatuwezi kuendelea na hali
hii ya kutiririsha maji kwenye makazi ya watu, ni bomu litakalolipuka hivi karibuni.
Kuna watoto wanacheza katika maeneo yale wanaweza kunywa au kunawa yale maji, kuna
mifugo inapita, inaweza kunywa yale maji, ni hatari kwa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Aliitaka
NEMC iangalie uwezekano wa kumpatia mtu binafsi aendeshe mfumo huo hata kama itabidi
asimamiwe na Halmashauri lakini kinachotakiwa ni kupatikana kwa mtu mwenye uwezo wa
kuendesha mfumo huo kwa utaalamu. Aliipa NEMC miezi miwili ili iwe imekamilisha utafiti
wake pamoja na kuangalia uwezekano wa kumpata mtaalamu wa kuifanya kazi hiyo.
Alitoa
pia mwezi mmoja kwa Manispaa ya Morogoro kuwa imetafuta eneo jipya na kubwa zaidi
kwa ajili ya kumwaga takataka kwani dampo lililopo katika kata hiyo linachangia uchafuzi
wa mazingira na kuleta kero kwa wananchi.
“Wakati ule dampo linaletwa huku
ilikuwa ni sahihi kwa sababu huku kulikuwa ni nje ya mji lakini kwa sasa siyo sahihi.
Nimemwambia Meya akae na watu wake wafikirie kujenga dampo jingine la kisasa... watafute
eneo kubwa na kuwe na mifumo ya kisasa,” alisema.
Kuhusu matumizi ya kuni katika
kiwanda hicho, Waziri Mkuu alisema hakubaliani kabisa na matumizi ya kuni kwa sababu
yanachangia uharibifu mkubwa wa mazingira. Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho, uendelee
na mpango wake mpya wa kutumia makaa ya mawe au hata kuangalia mpango wa kutumia umeme
utakaotokana na gesi.
“Najua kuna gharama katika kubadilisha mfumo wa boilers
zenu lakini matumizi ya tani 50 za magogo kwa siku hapana! Tani 50 nazilinganisha
na magunia 500 ya mahindi, sasa kwa miezi sita au kwa mwaka mmoja, mtatumia kuni kiasi
gani? Si Morogoro nzima itateketea? Alihoji Waziri Mkuu.
Akijitetea kuhusu
suala hilo, mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji alisema moto unaotokana na makaa
ya mawe hauna nguvu ya kutosha kuzalisha mvuke wa kuzalisha umeme wa kuendeshea mitambo
ya kiwanda hicho. “Tumeomba kwa mwaka mmoja tu tupewe ruhusa ya kuchanganya makaa
ya mawe na vipande vya miti hadi tutakapopata boilers mpya,” alisema.
Waziri
Mkuu alimweleza Bw. Dewji asubiri majibu ya maombi yake kutoka NEMC ambako maombi
hayo yalipelekwa lakini pia akawaonya viongozi wa NEMC kuwa makini wakati wanapitia
maombi hayo ili waweze kuwa na mbinu za kubainisha kama kweli vitatumika vipande vya
miti au watarudia utaratibu wao wa zamani wa kutumia magogo lakini wanayakata katika
vipande vidogo vidogo.
Hata hivyo, katika kikao hicho Meya wa Manispaa ya Morogoro,
Bw. Amiri Nondo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Said Amanzi walielezea kutoridhishwa
kwao na uhusiano uliopo baina ya uongozi wa kiwanda hicho na mamlaka zilizopo wakidai
kufungiwa mageti na kutotekelezwa kwa maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.
Waziri
Mkuu alimtaka mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji ajenge mahusiano mazuri na
uongozi wa mkoa kwa sababu viwanda vyake viko katika mkoa huo na hivyo hana budi kuzingatia
maslahi ya wakazi wa Morogoro kwanza. “Wao ni viongozi wa mkoa lakini pia ni wawakilishi
wa wananchi, kwa hiyo wanawajibika kwa wananchi, linapotokea jambo wao ndiyo wataulizwa
na wananchi,” alisisitiza.