2013-12-06 11:11:15

Tata Madiba atakumbukwa kwa kusamehe na kusahau bila kuweka kinyongo moyoni mwake!


Marehemu Nelson Mandela ni kiongozi aliyekuwa na busara na ukomavu, kiongozi ambaye kwa hakika ni kielelezo cha zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa watu wa nyakati hizi. Atakumbukwa kutokana na jitihada zake za kutaka kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini, waliokuwa wamegawanyika kutokana na ubaguzi wa rangi; ni kiongozi na mtetezi wa haki msingi za binadamu, aliyetanguliza utu wa watu kuliko hata masilahi yake binafsi, akawa ni mfano wa kuigwa dhidi ya ukoloni, ukandamizaji na ubaguzi wa rangi.

Ni sehemu ya salam za rambi rambi kutoka kwa Dr. Olav Tveit, Katibu mkuu wa Mabaraza ya Makanisa Ulimwenguni wakati huu dunia inapoomboleza kifo cha Mzee Madiba, kilichotokea Alhamisi, tarehe 5 Desemba, 2013 mjini Johanesburg, Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyeonesha moyo wa shukrani kwa wote waliosaidia kufanikisha mageuzi na uhuru wa kweli nchini Afrika ya Kusini.

Kanisa lilimsindikiza hata gerezani alipokuwa anatumikia kifungo cha maisha! Miaka 95 ya Mzee Madiba ni kielelezo cha utu na uhuru wa binadamu wote, atakumbukwa kwa kusamehe na kusahau bila kuweka kinyongo moyoni, jambo ambalo si rahisi sana kwa watu wa kizazi hiki wanaotaka kulipiza kisasi. Ni kiongozi na mfano wa kuigwa katika kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na utu wa mwanadmu.







All the contents on this site are copyrighted ©.