2013-12-05 08:38:23

Mkutano wa Makardinali unaendelea mjini Vatican


Makardinali walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kumsaidia kuchangia mawazo ili kufanya mageuzi ndani ya Kanisa wanaendelea na mkutano wao mjini Vatican. Makardinali wameendelea kushirikishana mang'amuzi na mawazo yao katika hali ya utulivu, ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa.

Kikao cha Jumatano asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko hakuweza kuhudhuria kutokana na sababu kwamba, alikuwa anaendesha Katekesi kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwa wingi mjini Vatican. Jumanne jioni, Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, alialikwa kuonana na kusalimiana na Makardinali hawa, kwani Askofu mkuu Parolin ni kati ya wasaidizi wakaribu sana wa Baba Mtakatifu.

Padre Federico Lombardi, SJ, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Makardinali katika mkutano wao, wanaendelea kupembua kwa kina na mapana kuhusu Mabaraza mbali mbali ya Kipapa na baadaye yatafuata mabaraza ya ushauri na hatimaye, taasisi za kipapa. Mzunguko huu wa kwanza unachambua mambo muhimu ambayo baadaye yatafanyiwa kazi kwa utekelezaji zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.