Miaka 50 ya Intermirifica: mwaliko wa kusikiliza, kujadiliana na kuwasiliana, ili
Kristo afahamike na kupendwa na wengi!
Mama Kanisa anaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
ulipochapisha waraka kuhusu njia za mawasiliano ya Jamii kwa Kilatini, Intermirifica.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii,
anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza
na kujadiliana ili kumpeleka Kristo kwa watu wote wanaokutana nao katika hija ya maisha
yao hapa duniani.
Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii katika Maadhimisho
haya, limezindua Mtandao wake mpya wa mawasiliano unaoweza kutembelewa kwa anuani
ifuatayo: www.intermirifica50.va. Kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaweza kupata
ujumbe huu kwa njia ya twitter kwa anuani ifuatayo: @pccs.va.
Wakati huo
huo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano kimeadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka
wa Intermirifica kwa Kongamano la kimataifa, kuhusu umuhimu wa njia za mawasiliano
katika maisha na utume wa Kanisa.